1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benazir Bhutto hatimaye azikwa.

28 Desemba 2007

Kiongozi wa upinzani Bibi Benazir Bhutto amezikwa rasmi kijijini kwao Ghari Khuda Baksh nchini Pakistan, huku waombolezaji wakiishutumu serikali ya rais Musharraf.

https://p.dw.com/p/ChWh
Mazishi ya waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhuto katika kijiji cha asili yake huko Ghari Khuda Baksh katika jimbo la Sindh.Picha: AP Photo/B.K.Bangash

Benazir Bhutto waziri mkuu wa zamani wa Pakistan hatimaye amezikwa rasmi , katika mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya waombolezaji katika kijiji cha Ghari Khuda Bakshi, huku vyombo mbali mbali vya habari vya kimataifa vikieleza hofu kubwa ya kuzuka kwa ghasia na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo inayomiliki silaha za kinuklia.

Sauti ya mgurumo wa watu ilitoka katika kundi la mamia kwa maelfu ya watu waliohudhuria mazishi baada ya mwili wa waziri mkuu wa zamani , marehemu Benazir Bhutto ulipowasili katika eneo la makaburi la familia yake katika kijiji cha Ghari Khuda Baksh katika jimbo la kusini la Sindh. Ndani ya jengo kubwa la kuzikia kiongozi wa kidini Mullah aliongoza sala ya mazishi , huku waombolezaji wakiwa wameinua mikono yao mbele ya nyuso zao wakisema Allahu Akhbar, Mungu mkubwa, mara tatu.

Machozi yaliporomoka katika uso wa mume wa marehemu Bhutto , Asif Zardari wakati mwili wa Bhutto ukishushwa kaburini, wakati mwanae Bilawal alionekana kuwa katika hali ya mshtuko mkubwa.

Nje ya jengo hilo kundi kubwa la watu lilikuwa likiimba maneno ya kuishutumu serikali ya rais Pervez Musharraf kwa kifo cha Bhutto kilichotokana na shambulio la bomu la kujitoa muhanga katika mkutano wa kampeni za uchaguzi uliofanyika katika mji wa kaskazini wa Rawalpindi jana mchana.

Mwangamizeni Musharraf, amemuua kiongozi wetu na tuyatima sasa, Mungu ashukuriwe Benazir alikuwa hana hatia, waliendelea kuimba.

Hapo mapema gari iliyokuwa imebeba mwili wa Benazir Bhutto katika jeneza lililofunikwa bendera ya rangi nyeusi, kijani na nyekundi ya chama cha Pakistan Peoples Party PPP, ilichukua saa mbili kukamilisha safari ya kilometa tano kutoka katika nyumba ya familia hadi katika mahali pa mazishi.

Wakati jeneza likipita katika makundi ya watu , maombolezaji wengi walilisogelea gari hilo, wakilia na kupiga vifua vyao katika hali kubwa ya huzuni.

Mbele ya eneo la makaburi , ambako baba yake Bhutto na kaka zake wawili pia wamezikwa, maelfu ya watu walijikusanya. Wengi wa waombolezaji hao walipepea bendera ya chama cha Bibi Bhutto. Akielezea kifo hicho kilichostua ulimwengu, msaidizi wa msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Tom Casey ameeleza masikitiko makubwa ya serikali yake kuhusiana na kifo hicho.

Hofu ya kuzuka kwa machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika Pakistan nchi inayomiliki silaha za kinuklia imeelezwa na vyombo vingi vya habari vya kimataifa baada ya kuuwawa kwa kiongozi huyo wa upinzani.

Kuuwawa kwa waziri mkuu huyo wa zamani , ambaye aliweza kurejea nchini mwake baada ya kuishi uhamishoni akiwania kushiriki katika uchaguzi mwezi ujao, ni msiba mkubwa kwa nchi hiyo ambayo tayari inakumbwa na matatizo kadha ya kiserikali, limeandika gazeti la Financial Times, gazeti la masuala ya kibiashara nchini Uingereza.