1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya dunia yawekeza kwa kampuni zinazokwepa kodi

12 Aprili 2016

Shirika la misaada la Oxfam limesema (11.04.2016) kiwango kikubwa cha mikopo inayotolewa na kitengo cha utoaji mikopo cha Benki ya Dunia Afrika inakwenda kwa makampuni yanayoficha mali zao katika maficho ya wakwepa kodi.

https://p.dw.com/p/1IU0y
Logo der Weltbank in Washington USA
Nembo ya Benki ya Dunia yenye makao yake makuu mjini Washington, MarekaniPicha: picture-alliance/dpa

Shirika hilo limesema asilimia 84 ya uwekezaji wa kitengo chake cha Utoaji mikopo, International Finance Coroporation, IFC, katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara mwaka 2015 ulikwenda kwa kampuni ambazo utumiaji wake wa maeneo ya kuficha fedha ili kukwepa kulipa kodi, hayana uhusiano bayana na kazi yao kubwa na kiwango cha chini cha uwazi.

Ikijibu ripoti hiyo IFC ilisema uchambuzi wa shirika la Oxfam umevurugwa na kwamba katika visa vyote kitengo hicho huzitaka kampuni zinazoendesha miradi yake kuheshimu sheria zinazotumika, ikiwa ni pamoja na sheria kuhusu kodi.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Oxfam, IFC iliwekeza zaidi ya dola bilioni 3.4 katika nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara mwaka 2015 na asilimia 75 ya kampuni 68 ilizozipa mikopo zilikuwa zikitumia maeneo yanayotumiwa na wakwepa kodi.

"Kwa kuruhusu uwekezaji katika maeneo hayo kitengo cha benki ya dunia hatimaye kinazinyima nchi masikini mapato zinayoyahitaji sana kupambana na umasikini na kukosekana usawa," alisema Nick Bryer, Mkuu wa Oxfam anayehusika na ukosefu wa usawa.

Lakini kitengo cha IFC kimesema shirika la Oxfam lilikuwa linatumia fikra isiyo sahihi kwamba kampuni zinazopatikana katika maeneo hayo bila shaka zilikuwa zikikwepa kulipa kodi.

"Ripoti hii inamaanisha kuwa mamlaka zote za nje au vituo vya fedha vya nje ni maeneo salama ya kodi, kwa kuwa tu ni nje, na kwamba uwekezaji katika biashara kubwa za kimataifa ni ukwepaji kodi," alisema Frederick Jones, msemaji wa IFC, wakati alipozungumza na Wakfu wa Thomson Reuters.

"Kuna matumizi halali ya mifumo inayopatikana katika visiwa. Matumizi sahihi ya vituo vya fedha katika maeneo hayo yanaweza kuongeza mtaji binafsi kwa ajili ya uwekezaji unaowasaidia watu masikini." akaongeza kusema katika maelezo yake aliyoyatuma kwa njia ya barua pepe.

Kwa mujibu wa shirika la Oxfam, eneo mashuhuri linalotumiwa na wateja wa kitengo cha benki ya dunia ni Mauritius, inayofahamika kwa kuziruhusu kampuni kuhamisha fedha kisiwani humo kabla kuzirejesha kama uwekezaji wa moja kwa moja, hali inayoruhusu faida kwa upande wa kodi.

Nyaraka za Panamana

Ripoti hiyo ilichapishwa baada ya ufichuzi wa vyombo vya habari kuhusu kampuni ya sheria ya Panama, Mossack Fonseca, iliyojikita na kazi ya kuanzisha makampuni katika maeneo ya visiwa.

Symbolbild Panama Papers Mossack Fonseca
Nyaraka za PanamaPicha: picture-alliance/maxppp/J. Pelaez

Nyaraka za Panama zilizofichuliwa yadaiwa zinaonyesha baadhi ya kampuni zinazoendesha shughuli zao katika maeneo hayo zilikuwa zikitumiwa kwa ulanguzi wa fedha, biashara ya silaha na dawa za kulevya na ukwepaji wa kulipa kodi.

Shirika la Oxfam limesema ingawa kitengo cha benki ya dunia, IFC, kinaongoza katika sekta ya kibinafsi linapokuja suala la ufichuzi, taarifa kuhusu inakokwenda asilimia zaidi ya hamsini ya ufadhili wake wa fedha, haziko wazi kwa umma kwa sababu ya madalali wajanja wanaozificha.

"Kitengo cha Benki ya Dunia hakitakiwi kujiingiza katika hatari ya kuzifadhili kampuni zinazokwepa kulipa kodi barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na ulimwenguni kote. Kinahitaji kuweka sheria kuhakikisha wateja wake wanaweza kuthibitisha wanalipa sehemu yao ya haki ya kodi," alisema Byer.

"Haina mantiki kwa kitengo cha benki ya dunia kutumia fedha kuziwezesha kampuni kuwekeza katika maendeleo huku kikifumbia macho ukweli kwamba kampuni hizi huenda zinazidanganya nchi masikini na kuzinyima mapato ya kodi yanayohitajika kupambana na umasikini na kukosekana usawa," amesema Susana Ruiz, mshauri wa masuala ya kodi wa shirika la Oxfam.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi zinazoendelea hupoteza takriban dola bilioni 100 ya mapato yanayotokana na kodi kwa mwaka kwa sababu ya ukwepaji kodi wa makampuni.

Mwandishi:Josephat Charo/rtre/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga