1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Ulaya na nchi za G7 kushirikiana kustawisha uchumi

8 Agosti 2011

Nchi zilizostawi kiviwanda G7 zimeahidi kuchukua hatua ya pamoja kurejesha utulivu katika masoko ya fedha. Benki Kuu ya Ulaya imesema itanunua dhamana za serikali katika kanda ya Euro, ili kuudhibiti mzozo wa madeni.

https://p.dw.com/p/12CoX
Rais wa benki kuu ya Ulaya, Jean-Claude TrichetPicha: dapd

Viongozi wa kundi la G7 linalojumuisha Marekani, Ujerumani, Uingereza, Canada, Ufaransa,Italia na Japan wamesema, wanapaswa kuwa na msimamo mmoja katika masoko ya fedha, kwani vinginevyo kutaathiri vibaya sana uthabiti wa uchumi na fedha. Kufuatia tangazo hilo, Benki Kuu ya Ulaya ECB, iliashiria kuwa itaanza kununua dhamana za Italia na Uhispania ili kurejesha imani ya wawekezaji.

Rais wa ECB, Jean-Claude Trichet, amesema, benki hiyo inaunga mkono hatua mpya zinazochukuliwa na Italia na Uhispania kufanya mageuzi katika mifumo ya fedha ili kupunguza matumizi ya serikali. Nchi hizo mbili ni miongoni mwa zile zinazokabiliwa na madeni katika kanda inayotumia sarafu ya Euro barani Ulaya. Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi alitangaza hatua mpya za kupunguza haraka nakisi katika bajeti ya serikali na kuharakisha mageuzi katika sekta ya uchumi. Ahadi za G7 na Benki Kuu ya Ulaya zinakuja wakati thamani ya hisa ikiendelea kuporomoka katika masoko ya fedha duniani.

China ina wasiwasi

Hali hiyo inaitia wasiwasi China kwani imedhamini mikopo ya Marekani na nchi nyingine kwa mabilioni ya dola. China, mara nyingine tena imewakosoa wanasiasa wa Marekani na Ulaya kwa kutokuwa na ujasiri wa kuyakabili matatizo ya deni kwa dhati. Gazeti la Peoples Daily, linalomilikiwa na serikali ya China, limeonya kuwa iwapo Marekani, Ulaya na mataifa mengine yenye uchumi imara, yatashindwa kuwajibika na yataendelea kubishana kwa sababu ya maslahi binafsi, hiyo itazuia maendeleo imara katika uchumi wa kimataifa.

US-Finanzminister Geithner
Waziri wa fedha wa Marekani, Timothy GeithnerPicha: picture alliance/dpa

Wasiwasi ulizidi katika masoko ya fedha, baada ya shirika la Standard & Poor´s linalotathmini uwezo wa nchi kulipa madeni, kuamua kuishusha Marekani kutoka kiwango cha juu kabisa cha kuaminiwa kulipa madeni. Uamuzi huo umekosolewa vikali na waziri wa fedha wa Marekani, Timothy Geithner. Amesema huo ni uamuzi mbaya na usio na maana na wala hautoathiri imani ya wawekezaji kuhusu hisa za serikali ya Marekani.

Lakini masoko ya fedha duniani yatataka pia kujua vipi Marekani inapanga kupunguza deni lake lililopindukia dola trilioni 14, bila ya kuathiri uchumi wa nchi hiyo unaoimarika pole pole.

Mwandishi: Martin,Prema/ rtre

Mhariri: Josephat Charo