1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

150708 USA Finanzkrise

Charo, Josephat15 Julai 2008

Kwa mara ya pili katika mwaka huu mfumo wa fedha wa Marekani unakaribia kuporomoka.

https://p.dw.com/p/Ed5k
Waziri wa fedha wa Marekani Henry PaulsonPicha: AP

Mnamo siku ya Jumapili tarehe 16 mwezi Machi mwaka huu benki kubwa ya JP Morgan Chase kupitia msaada wa benki kuu ya Marekani iliinunua benki ya uwekezaji ya Bear Stearns na kwa hiyo kuzuia kuporomoka kwa masoko ya hisa. Sasa mzozo mwingine mpya unayakabili masoko ya hisa ya Marekani. Wateja wanakimbilia mabenki na kuchukua pesa zao.

Hali hii inafanana na wakati kulipotokea mzozo mkubwa wa kifedha miaka 80 iliyopita. Bila shaka hofu katika masoko ya hisa ya Wall Street ni dhahiri. Na hata waziri wa fedha wa Marekani na gavana wa benki kuu wanaonekana kuwa na wasiwasi mkubwa.

Siku chache tu baada ya waziri wa fedha Henry Paulson kutangaza rasmi kwamba fedha za benki za kutoa mikopo ya nyumba za Fannie Mae na Freddie Mac ziko salama, alishauriana na benki kuu mwishoni mwa juma lililopita kuhusu mpango wa kuziokoa benki hizo.

Baadaye benki ya Fannie Mae na Freddie Mac zilipewa ruhusa ya kukopa zaidi kupita kiwango zinachotakiwa kukopa katika benki kuu kama iliyokuwa katika mzozo ulioikabili benki ya uwekezaji ya Bear Stearns.

Na kwa upande mwingine bunge la Marekani linatarajiwa katika siku chache zijazo kuidhinisha serikali ya Marekani iziuze hisa zozote itakazo za benki za Fannie Mae na Freddie Mac.

Kwa mujibu wa Sean Egan, mshirika wa wakala wa Eagen Jones, hiyo ni hatua inayofaa kuchukuliwa.

´Ni jambo la kutuliza wasiwasi kwamba waziri wa fedha Paulson amejitolea kuingilia kati na kusaidia. Lakini hata hivyo kulazimika kwake kuingilia kati, kunadhihirisha vipi tatizo la kiuchumi lilivyokuwa kubwa katika mwaka mmoja au miaka miwili iliyopita.´

Martin Mayer, mtaalamu katika benki kuu ya Marekani anayeifanyia kazi taasisi ya kibinafsi ya Brookings mjini Washington na muandishi wa vitabu kadhaa kuhusu benki kuu ya Marekani anapinga hatua ya kuuza hisa za benki za Freddie Mac na Fannie Mae.

´Sijui ni kitu gani hasa. Ni kitendo kinachodhihirisha wasiwasi mkubwa. Sidhani kama kulikuwa na haja kufanya hivyo. Benki za Fannie Mac na Freddie Mae zinaweza kukopa hadi dola bilioni 2,5 katika hazina kuu. Kiwango hiki kinaweza kuongezwa kiurahisi na hicho ndicho kitu pekee kinacholazimika kufanywa.´´

Freddie Mac na Fannie Mae zinamiliki au kudhamini takriban nusu ya mikopo ya kununua nyumba nchini Marekani. Thamani yake inasemekena ni dola bilioni tano, mara mbili ya pato jumla ya taifa la Ujerumani.

Je hili liliweza vipi kutokea? Benki ya Freddie Mac na Fannie Mae zilichukua dhamana ya mikopo ya benki nyengine na kuchukua hati za uklopeshaji na kuziuza kwa wawekezaji zikiwemo benki za Ujerumani. Kuporomoka kwa masoko ya mikopo ya nyumba kumesababisha thamani ya hati hizo za ukopeshaji kupungua sana.

Bibi huyu amekuwa akifuatili kwa karibu sakata la benki za mikopo ya nyumba ikiwa linazusha hisia za mdororo mkubwa wa shughuli za kiuchumi. Kuhusu hisia zake ikiwa hilo litatokea tena anasema

``Kusema kweli sidhani hali ni mbaya sana lakini pengine ni kitu kinachokuja. Na nadhani wanajaribu kukabiliana na hali hiyo kabla benki kuporomoka kabisa.´´

Je bibi huyu anahofia pesa zake katika benki?

``Aaaah mimi sina hofu sana kuhusu pesa zangu zilizo katika benki. Wasiwasi wangu mkubwa ni kuhusu pesa zangu nilizowekeza. Mambo kwa sasa yanaporomoka kwa kasi kubwa mno.´´

Masoko ya hisa ya Marekani yanapitia wakati mgumu na mpaka sasa waziri wa fedha na gavana wa benki kuu hawajafaulu kuyadhihirishia masoko hayo na wawekezaji kwamba hao ndio mabwana wa swala hilo.