1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bensouda alia na Umoja wa Afrika

Admin.WagnerD29 Mei 2013

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, Fatou Bensouda amewajibu wakosoaji, baada ya Umoja wa Afrika kuishtumu mahakama hiyo kwa ubaguzi.

https://p.dw.com/p/18g5G
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Fatou Besnouda.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Fatou Besnouda.Picha: AFP/Getty Images

Mwendesha Mashataka huyo hakutaja kundi maalumu, lakini matamshi yake yamekuja siku moja tu baada ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika kusema kwamba ICC ilikuwa inalilenga bara hili kwa misingi ya rangi. Alipoulizwa na mwanadiplomasia kutoka Afrika kuhusu sauti hizo zinazohoji mbinu za ICC, Bensouda aliuambia mkutano uliyofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kuwa sauti hizo zinafahamika vizuri, na kwamba ni za wale wanaotaka kuwalinda waliotenda uhalifu, na wala sio sauti zinazowaunga mkono waathirika wa uhalifu huo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wanaotaka dhidi yao isitishwe katika ICC.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wanaotaka dhidi yao isitishwe katika ICC.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kenya yawa mwiba mchungu

ICC inakabiliwa na shinikizo kubwa la kidiplomasia kuhusiana na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu yanayowakabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto, ambayo yanahusiana na machafuko ya kisiasa ya mwaka 2008, wakati hakuna kati ya wawili hao aliekuwa ofisini. Mkutano wa Umoja wa Afrika siku ya Jumatatu ulitaka mashtaka ya ICC yasitishwe, na Kenya imetuma maombi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufuta kesi hiyo.

Bensouda alisema wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu upotevu uliopangwa, ulioandaliwa na Ufaransa na Argentina, kuwa dunia haipaswi kutumia kile inachokifanya ICC kuigeuzia kibao. Alisema waathirika wa kweli wa uhalifu ni waathirika wa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya halaiki, na wala sio wale wanaochochea uhalifu huo, akiongeza kuwa sauti zinazosikika kwa sasa, ni zile zinazojaribu kuwalinda wale walioshiriki uhalifu huo.

"Nadhani hii ni dharau kwa waathrika hao. Hili halipaswi kuwa linatokea, na yeyote anaehusika na kushughulikia uhalifu wa aina hii - dhidi ya maelfu kwa maefu ya waathirika, waathirika wa Kiafrika, anapaswa kuguswa na kile kinachotokea hivi sasa," alisema mwanamama huyo kutoka Gambia, na kuapa kuwa ICC itaendelea kuwa huru, kutoegemea upande wowote, kutekeleza sheria bila kujali mashinikizo ya kisiasa na mengine.

Viongozi wa Afrika wakiwa katika mkutano wao mjini Addis Ababa Jumatatu wiki hii, ambapo walikubaliana kwa pamoja kuishinikiza ICC kufuta kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto.
Viongozi wa Afrika wakiwa katika mkutano wao mjini Addis Ababa Jumatatu wiki hii, ambapo walikubaliana kwa pamoja kuishinikiza ICC kufuta kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto.Picha: picture-alliance/dpa

Afrika ndumila kuwili?

Serikali za Kiafrika mara nyingi huelezea hasira kwamba uchunguzi wote wa ICC unalenga bara hilo. Lakini karibu kesi zote nane za uchunguzi - kuanzia Uganda hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mali ziliwasilishwa katika mahakama hiyo na nchi za Afrika zenyewe.

Mataifa 43 ya Afrika yalisaini mkataba wa Rome uliyoanzisha mahakama ya ICC na mataifa 34 yameridhia mktaba huo. Hii inaifanya Afrika kuwa kanda yenye uwakilishi mkubwa zaidi katika uanacham wa mahakama hiyo. Tiina Intelmann, rais wa baraza la nchi 122 wanachama wa ICC, alikiri kuwa dhana kuwa uchunguzi wa mahakama hiyo unalenga Afrika peke yake, imesababisha ugumu katika uhusiano wa ICC na mataifa ya Afrika.

"Pamoja na hayo, tusisahau kuwa kuliangazia bara la Afrika kwa sasa kunamaanisha pia kuwaangazia waathirika wa Kiafrika," alisema Intelmann katika maoni. Mfuko ulioanzishwa na mkataba wa ICC umewasaidia karibu waathirika 8000 wa uhalifu wa kikatili. "Ni haki kusema kuwa bila shughuli za mfuko huo, waathirika wote hao wa kiafrika wangepata msaada kidogo sana au kutopata kabisaa," aliongeza Intelmann.

Picha hii ni kumbukumbu ya mwaka 2008 nchini Kenya, ambapo vurugu zilizosababishwa na uchaguzi ziliua watu wasiopungua 1200. Ni vurugu hizo zinazowandama Kenyatta na Ruto katika mahakama ya ICC hivi sasa.
Picha hii ni kumbukumbu ya mwaka 2008 nchini Kenya, ambapo vurugu zilizosababishwa na uchaguzi ziliua watu wasiopungua 1200. Ni vurugu hizo zinazowandama Kenyatta na Ruto katika mahakama ya ICC hivi sasa.Picha: AP

Gazeti Kenya latakiwa kumuomba radhi Kenyatta

Wakati huo huo, gazeti moja nchini Kenya, limeamriwa na Baraza la habari nchini humo kuomba radhi katika tovuti yake kwa siku saba mfululizo, kutokana ma maoni yaliyochapishwa yakifananishan uchaguzi wa Kenyatta na kuibuka kwa Adolf Hitler nchini Ujerumani. Mlinganisho huo umemkasirisha hasa rais Kenyatta, wakati kesi yake ikitarajiwa kuanza mwaka huu katika mahakama ya ICC.

Makala ya maoni iliyoandikwa na mwandishi wa makala Jerry Okungu na kuchapishwa Februari 2012, ililinganisha uwezekano wa kuchaguliwa kwa Kenyatta na kuibuka kwa Hitler, na ilijikita hasa katika matukio yaliyopelekea kuteuliwa kwake kama Kansela mwaka 1933.

Okungu ambae alionya kuwa Kenyatta angeiendesha nchi kwa manufaa yake binafsi na ya washirika wake, anasema alimaanisha tu kulinganisha kuibuka kwa wanasiasa hao wawili, na si kulinganisha matendo ya Kenyatta na Hitler.

Makao makuu ya mahakama ya ICC yaliyoko mjini The Hague, Uholanzi.
Makao makuu ya mahakama ya ICC yaliyoko mjini The Hague, Uholanzi.Picha: Getty Images

Kenyatta alisema laazima apambane na machapisho kama hayo kwa sababu ndiyo yanayotumika na ICC dhidi yake. Baraza la habari lilisema katika ripoti yake kuwa machapisho hayo yanamlinganisha Kenyatta na Hitler, si tu katika masuala ya umaarufu, lakini katika muktdha wa uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman