1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Jeshi la Ujerumani kubaki Afghanistan.

21 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzq

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung amesema kuwa jeshi la nchi hiyo Bundeswehr linaendelea kuwapo nchini Afghanistan licha ya vifo vya wanajeshi wake watatu wa kulinda amani katika shambulio la kujitoa muhanga katika mji wa kaskazini wa Kunduz siku ya Jumamosi.

Akizungumza katika mahojiano ya radio , Jung amesema Ujerumani haitakubali kutishwa ili iondoe majeshi yake kwa mashambuli kama hayo.

Msemaji wa jeshi la Ujerumani Wilfried Stolze amesema pia kuwa Ujerumani inapaswa kuendelea na mikakati ya kuwapo Afghanistan ikiwa jumuiya ya kimataifa inahitaji kufanikiwa katika lengo lake.

Vifo hivyo vitatu vya wanajeshi wa Ujerumani vinafikisha idadi ya wanajeshi 21 ambao wamepoteza maisha yao nchini Afghanistan tangu mwaka 2002.

Wakati huo huo wanne katika ya wanajeshi watano wa Bundeswehr ambao wamejeruhiwa katika shambulio hilo wamerejeshwa nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

Ujerumani ina kiasi cha wanajeshi 3,000 wanaotumikia jeshi la NATO nchini Afghanistan.