1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Kansela Merkel akasirishwa na picha za wanajeshi wa Ujerumani

25 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCzK

Wanajeshi wawili wa Ujerumani wameanza kuhojiwa leo baada ya gazeti moja hapa nchini kuchapisha picha za wanajeshi wa Ujerumani wakiwa na bufuru walipokuwa katika doria nchini Afghanistan.

Gazeti la Bild limechapisha picha tano za wanaume waliovaa sare za jeshi la Ujerumani wakicheza na bufuru hilo kwenye magari ya jeshi. Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amezieleza picha hizo kuwa za kushtusha na kuudhi.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Thomas Steig, amesema picha hizo zinayaharibia sifa majeshi ya Ujerumani na taifa zima kwa jumla.

Msemaji wa jeshi la ISAF nchini Afghanistan, Luke Knitting, amesema jeshi hilo litashirikiana na wizara ya ulinzi ya Ujerumani na kuisadia katika uchunguzi wake.

´Tutashirikiana na kusaidia kadri itakavyowezekana katika kila hali ambayo wizara ya ulinzi ya Ujerumani itaona inaweza kusaidia.´

Wakati alipoamuru uchunguzi ufanywe kuhusiana na picha hizo waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, amesema tabia kama hiyo miongoni mwa wanajeshi wa Ujerumani haiwezi kuvumiliwa.