1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Kansela wa Ujerumani akamilisha ziara yake ya mashariki ya kati

3 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCCx

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekamilisha ziara yake ya siku tatu katika mashariki ya kati.

Bibi Merkel katika hatua za mwisho wa ziara yake alikitembelea kikosi cha wanamaji wa Ujerumani kinacho tekeleza majukumu ya kupiga doria katika pwani ya Lebanon.

Kansela Angela Merkel amepongeza kazi inayofanywa na kikosi cha Ujerumani chenye askari 1600 kinachoongoza kikosi cha wanamaji cha kulinda amani cha umoja wa mataifa kilichopewa jukumu hilo baada ya kumalizika vita kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hezbollah.

Awali bibi Merkel alikutana na waziri mkuu wa Lebanon Fuoad Siniora na katika mkutano wao kansela wa Ujerumani alisisitiza umuhimu wa kuwepo uhuru nchini Lebanon na wakati huo huo kuitolea mwito nchi jirani ya Syria itoe ushirikiano kwa maafisa wa umoja wa mataifa wanaochunguza mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri aliyeuwawa miaka miwili iliyopita.