1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Maandamano yafanyika kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani

1 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC5S

Maandamano ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi yamefanyika kote duniani huku mengi yakikumbwa na machafuko na visa vya watu kukamatwa na polisi.

Mjini Berlin hapa Ujerumani polisi wamewakamata watu 68 mapema leo kwenye machafuko ya sikukuu ya wafanyakazi. Msemaji wa polisi mjini humo amesema watu waliwarushia chupa na mawe maofisa wa usalama lakini hakuna aliyejeruhiwa kwenye vurugu hizo.

Watu hao walikamatwa katika wilaya ya mashariki ya Friedichshain mjini Berlin wengi wao wakiwa vijana waliokuwa wamelewa.

Msemaji wa polisi mjini Berlin Bernard Schodrowski amesema wamekuwa wakishudia tangu miaka 20 iliyopita jinsi tarehe mosi mwezi Mei inavyokuwa na machafuko mjini Berlin na wamejaribu mbinu zote bila mafanikio.

´Tumekuwa wabaya, tumewakataza watu wasifanye lolote na tumewaruhsu pia wafanye watakavyo. Lakini hatukufanikiwa. Sasa tunachukua tahadhari kuwaruhusu watu wafanye watakavyo kwa amani, ila wasiwaudhi watu wengine. Tunakabiliana na uvunjaji wowote wa sheria.´

Duru za polisi mjini Berlin zinasema maandamano ya mwaka huu hayakuwa na machafuko makubwa kama ya miaka iliyopita.

Nchini Uturuki polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji na kuwakamata viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliokuwa wakishiriki kwenye maandamano.

Na huko nchini Urusi, malefu ya waandamani walijitokeza kutaka nyongeza za mishahara na malipo zaidi ya uzeeni katika maandamano yaliyokwepa kuikosoa serikali ya rais Vladamir Putin.