1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Marekani yakanusha Ujerumani ilitaka kumrejesha nyumbani Kurnaz

2 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCNC

Afisa wa zamani wa serikali ya Marekani, Pierre Richard Prosper, amesema Ujerumani haikutaka raia wake wa asili ya kituruki, Murat Kurnaz, aachiliwe huru kutoka jela ya Guantanamo Bay alikokuwa akizuiliwa.

Aidha afisa huyo amesema Ujerumani haikuwasilisha ombi lolote wakati alipokuwa katika uongozi.

´Kama Ujerumani ingesema mwaka wa 2002 kwamba ilitaka kumchukua Kurnaz, mimi kwa mujibu wa maagizo ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani wakati huo, Colin Powell, na rais wa Marekani, ningefanya mazungumzo na serikali ya Ujerumani juu ya masharti ya kurudishwa kwa Kurnaz.´

Matamshi haya yanatofautiana na madai yaliyotolewa na serikali ya zamani ya kansela Gehard Schroder kwamba ilifanya juhudi za kutaka Kurnaz aachiliwe huru kutoka jela ya Guantanamo.

Prosper, ambaye alikuwa afisa aliyesimamia kesi za uhalifu wa kivita kati ya mwaka wa 2002 na 2005, alikuwa akizungumza jana katika runinga ya Monitor.