1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Schäuble ataka ndege zilizotekwa nyara zitunguliwe

3 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdq

Licha ya tofauti zilizopo katika serikali ya muungano, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble wa chama cha CDU anashikilia mpango wake wa kuruhusu ndege za abiria zilizotekwa nyara zitunguliwe iwapo zitakuwa tisho la kigaidi.

Msemaji wa serikali mjini Berlin amesema wizara husika zinalidurusu pendekezo hilo, litakalosababisha katiba ya Ujerumani ibadilishwe. Chama cha Social Democrats, SPD na vyama vya upinzani vinapinga pendekezo hilo.

Waziri Schaüble anahoji kuwa tisho la ndege iliyotekwa nyara linatakiwa kuchukuliwa kama chanzo cha shambulio. Thuluthi mbili ya wabunge wanahitajika kuibadili katiba ya Ujerumani.

Wakati haya yakiarifiwa muongozaji mashtaka wa mjini Nuremberg ameanza kuchunguza ikiwa kampuni ya Siemens ya Ujerumani ilivunja sheria za biashara ya kimataifa kwa kuilipa serikali ya Irak chini ya utawala wa Saddam Hussein ili ishikiri katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa mafuta kwa chakula.

Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa wa mwaka juzi ulidhihirisha kuwa kampuni zaidi ya 2,000 ziliihonga serikali ya Irak ili zishiriki katika mpango huo.