1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Steinmeier ashtushwa na vitisho vya wateka nyara.

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKK

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameeleza kushtushwa kwake juu ya video iliyoonekana katika mtandao wa internet ikionyesha mateka wawili raia wa Kijerumani na vitisho vya kuuwawa vilivyotolewa na watekaji nyara waliowakamata nchini Iraq mwezi uliopita.

Steinmeier amesema kuwa kundi la kushughulikia mizozo katika wizara yake litafanya kila linalowezekana kuweza kupata kuachiwa kwa mwanamke wa Kijerumani mwenye umri wa miaka 61 pamoja na mtoto wake mkubwa.

Katika video hiyo , wateka nyara hao wanaotoka katika kundi ambalo halifahamiki sana linalojiita mshale wa wanyoofu, wametishia kuwauwa mateka wao katika muda wa siku kumi hadi pale Ujerumani itakapoondoa wanajeshi wake 3,000 nchini Afghanistan.

Siku ya Ijumaa bunge la Ujerumani liliamua kutuma wanajeshi 500 zaidi pamoja na ndege sita za upelelezi chapa Tonado nchini Afghanistan. Wapiganaji nchini Iraq katika ujumbe kupitia video ya pili pia wametishia kushambulia Austria ambayo inamaafisa watano nchini Afghanistan katika eneo la Kabul.