1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN : Ujerumani yahimiza utafiti bora wa UKIMWI

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKA

Waziri wa Afya wa Ujerumani Ulla Schmidt amesema mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yanapaswa kuimarisha uratibu katika juhudi zao za kutengeneza chanjo dhidi ya virusi vya HIV na UKIMWI.

Schmidt atasimamia mkutano wa kimataifa juu ya virusi vya HIV na UKIMWI katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Bremen hapo kesho.Amesema amekuwa na mazungumzo na wahusika wakuu katika viwanda vya madawa juu ya suala la bei za madawa ya matibabu ya UKIMWI.

Ujerumani hivi sasa ni rais wa Umoja wa Ulaya na wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda Duniani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Afrika na janga la UKIMWI ambalo limeliathiri vibaya bara hilo litakuwa mojawapo ya masuala makuu ya kuzingatiwa na Ujerumani wakati wa urais wake wa Kundi la Mataifa Manane.