1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Usalama wa mitambo ya nyuklia uimarishwe zaidi

19 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBhB

Waziri wa mazingira wa Ujerumani,Sigmar Gabriel anataka hatua kali zaidi za usalama zichukuliwe katika mitambo ya nishati ya nyuklia nchini Ujerumani.Ametamka hayo kufuatia ajali mbili zilizotokea kwenye mitambo ya nishati ya nyuklia nchini Ujerumani na kujiuzulu kwa meneja wa ngazi ya juu wa mtambo wa Vattenfall,ulio tawi la kampuni ya Kiswidi.Siku ya Jumatano,Klaus Raucher alijiuzulu kama kiongozi mmojawapo wa mitambo minne mikuu.Kampuni ya Vattenfall imekosolewa sana kuwa ilificha mambo mengi,baada ya kutokea dosari za kiumeme na transfoma moja kushika moto na hivyo mitambo kulazimika kufungwa kwa muda, hapo tarehe 28 mwezi Juni.

Waziri Gabriel amesema,haitoshi kubadilisha mameneja,bali makampuni husika yanapaswa kuachilia mbali mitambo iliyozeeka na badala yake itumie mitambo mipya iliyo na usalama bora zaidi. Makundi yanayotetea mazingira vile vile yametoa wito wa kuifunga mitambo ya zamani.