1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin. Wabunge washambulia uamuzi wa Ufaransa kuisaidia Libya kujenga kinu cha kinuklia.

28 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBeb

Shutuma kali dhidi ya mipango wa Ufaransa kujenga kinu cha kinuklia nchini Libya zinazidi kuongezeka nchini Ujerumani.

Reinhard Bütikofer , rais mwenza wa chama cha walinzi wa mazingira cha Greens , ameuita uamuzi huo kuwa harakati hatari za kiuzalendo zinazofanywa na rais huyo wa Ufaransa Nocolas Sarkozy.

Amesema kuwa mtazamo wa Sarkozy ni wa hatari. Umejengeka katika misingi ya kiuzalendo na kwamba kwa hakika hauko katika viwango vya mtazamo wa mataifa ya Ulaya.

Mbunge mwengine wa Ujerumani amemshutumu Sarkozy kwa kutoshauriana na wanachama wengine 26 wa umoja wa Ulaya. Siku ya Alhamis Sarkozy alitia saini taarifa ya maelewano kwa ajili ya makubaliano ya ujenzi wa kinu cha nishati ya kinuklia nchini Libya wakati wa ziara yake mjini Tripoli.

Wanasiasa wengine kutoka vyama viwili vinavyounda serikali ya Ujerumani wamesema kuwa mradi wa nishati ya kinuklia na nchi ambayo ni hivi karibuni tu ilimaliza miaka kadha ya kutengwa ni mapema mno na hatari sana. Miaka minne iliyopita , kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi alitangaza kuwa anafutilia mbali mradi wake wa silaha za kinuklia, kemikali na kibiolojia.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa aliwasili jana Ijumaa nchini Gabon kwa ziara ya saa tisa nchini humo, ikiwa ni kituo cha mwisho katika ziara yake ya mataifa ya eneo la kaskazini ya jangwa la Sahara.