1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni Mkenya wa kwanza kushinda mbio hizo fupi

26 Agosti 2015

Mkenya Nicholas Bett alinyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 400 kuruka viunzi kwa kutumia muda wa sekunde 47.79 katika mashindano ya ubingwa wa dunia mjini Beijing, China

https://p.dw.com/p/1GLX2
China Beijing 2015 IAAF Weltmeisterschaft Nicholas Bett
Picha: picture-alliance/dpa/F. Robichon

Ilikuwa medali ya kwanza ya Kenya katika mbio fupi katika mashindano ya dunia. Bett sasa ni mwanariadha wa pili Afrika kuwahi kushinda mbio hizo katika mashindano ya ulimwengu baada ya Samuel Matete wa Zambia aliyeshinda katika mashindano ya Tokyo mwaka wa 1991

Raia wa Urusi Denis Kudryavtsev alichukua medali ya fedha huku Jeffery Gibson wa Bahamas akimaliza wa tatu.

Wakati huo huo, Bingwa wa Olimpiki Mkenya David Rudisha alinyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 800 katika mashindano ya riadha ya dunia ya IAAF yanayoendelea mjini Beijing, China

Bingwa huyo wa Olimpiki na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio hizo ambaye pia alishinda taji la ulimwengu mwaka 2011, aliongoza kutoka hadi mwisho katika muda wa dakika 1 sekunde 45.84 mbele ya mwanariadha wa Poland Adam Kszczot.

Amel Tuka wa Bosinia Haerzegovina ambaye aliweka muda bora mwaka huu aliridhika na medali ya shaba. Mbio hizo hata hivyo zilikosa msisimuko wake kutokana na kukosekana mwanariadha wa Botswana Nijel Amos na Muethiopia Mohammed Aman ambao walishindwa kufuzu katika fainali.

Kwingineko, mwanariadha wa Ethiopia Genzebe Dibaba alichukua dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake.

Faith Chepng‘etich Kipyegon alichukua nafasi ya pili huku Sifan Hassan wa Uholanzi akimaliza wa tatu.

Kufikia sasa, Kenya inaongoza msimamo wa medali ikiwa na jumla ya tisa, nne za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba. Uingereza ni ya pili na dhahabu tatu ikifuatwa na Jamaica na dhahabu mbili. Ujerumani ni ya nne na dhahabu moja.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Daniel Gakuba