1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bhutto amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani

Jane nyingi9 Novemba 2007

Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Benazir Bhutto amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kumzuia kuongoza mkutano mkubwa hivi leo uliolenga kupinga hatua ya rais Musharraf kutangaza hali ya hatari. Huku hayo yakijiri aliyekuwa rais wa afrika kusini Nelson Mandela na aliyekuwa rais wa marekani Jimmy Carter wamemshtumu vikali Rais Musharraf kwa kuendelea kushikilia msimamo wake wa hali ya hatari.

https://p.dw.com/p/C772
Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Benazir Bhutto
Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Benazir BhuttoPicha: AP

Mamia ya polisi walizingira nyumba ya Bhutto mjini Islamabad saa kadhaa kabla ya muda aliyotarajiwa kuondoka ili kuongoza mkutano katika eneo jirani la Rawalpindi. Wafuasi wake elfu tatu pia walijipata mashakani kwani walitiwa mbaroni. Hali hii huenda hata ikachochea zaidi mgogoro ambao umekumba Pakistan taifa pekee la kiislamu lililo na silaha za kinuklia.Kwa Rais Musharraf huu ni wakati mgumu katika uongozi wake tangu alipochukua madaraka miaka minane iliyopita kufuatia mapinduzi.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kile maafisa wa serikali walidai maisha ya Bhutto kuwa hatarini. Hata hiyo viongozi wa chama cha Pakistan Peoples party anachotoka Bhutto walisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria hasa kwa kiongozi mwenye kuzingatia democrasia.

Karibu wafanayikazi 200 wa chama PPP, wakiwemo wanawake kadhaa waliingizwa katika magari ya idara ya magereza yaliyokuwa nje ya nyumba ya Bhutto baada ya kuanza kutoa matamshi ya kumsifu bhutto huku wakiwa wamebeba mabango. Karibu wafuasi elfu 3 wa chama cha PPP wamezuiliwa katika siku za hivi karibuni ,huku polisi wakisema ni karibu elfu 1 pekee.

Licha ya funununu za kugawana madaraka kati ya rais Musharraf na Bi Bhutto, Bhutto alitangaza kuandaa mkutano huo wa leo wa kupinga hatua ya Rais Musharraf kutangaza hali ya hatari jumamosi iliyopita .Baada ya kutangazwa kwa hali hiyo ya hatari mikutano ya kisiasa ilipigwa marufuku, kusitishwa kwa katiba, jaji mkuu kufutwa kazi na sheria kali kutolewa dhidi ya wanahabari.

Uchaguzi uliotarajiwa kufanyika mwezi januari mwaka ujao ulisongezwa hadi kati mwa mwezi Februari."Tulijaribu kumshawishi Bhutto kutoandaa mkutano huo lakini hakukubali,hatukuwa na namana nyingine ila tu kutekeleza kikwazo hicho"..amesema afisa mmoja mkuu wa polisi.

Serikali imewapaleka wanajeshi elfu 6 kuzuia Mkutano huo katika eneo la Rawalpindi,kwa kuzingira eneo ambalo Bhutto na wafuasi wake walitarajiwa kukutana.

Polisi walikuwa wametoa tahadhari kuwa kuna karibu walipuaji wa kujitoa mhanga wanane walioko katika mji huo wa Rawalpindi,na hivyo kuleta hali ya wasiwasi kuhusu kufanyika kwa shambulizi jingine kama lile la mashambulizi mawili kwa pamoja na walipuaji wa kujitoa mhanga yaliyofanyika october 18 wakati wa sherehe za kumkaribisha Bhutto nyumbani baada ya kuwa uhamishoni kwa miaka mitano.Wakati wa mshambulizi hayo watu 139 waliuawa.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha kimataifa cha BBC Bhutto alisema ahadi ya rais Musharraf kuandaa uchaguzi kati mwa mwesi februari na kung'atuka madarakani kama mkuu wa majeshi sio tosha katika kutatua mgogoro ambao umekumba Pakistan.

Kundi la waliokuwa viongozi akiwemo Nelson Mandela wa Afrika kusini na Jimmy carter wa Marekani wamemshtumu rais Musharraf kwa kutangaza hali ya hatari nchini Pakistan. Walisema hali hiyo imesababaisha kuvunjwa kwa haki za kibinadamu miongoni mwa wanaharakati, waadishi habari na wapinzani. Kundi hilo la viongozi wakongwe lilibuniwa mapema mwaka huu katika juhudi za kutumia ushawishi wao kupunguza migogoro katika mataifa mbalimbali duniani.

Arch bishop Desmond Tutu ,aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Koffi Annan, Nelson Mandela na Jimmy Carter ni miongoni mwa wanachama wa kundi hilo.