1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bhutto ataka kuunda muungano wa upinzani

Josephat Charo14 Novemba 2007

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto, anatafuta kuunda muungano wa upinzani dhidi ya rais Pervez Musharraf. Bi Bhutto amemkosoa vikali rais Musharraf kwa kutangaza hali ya hatari nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/CH6u
Benazir Bhutto
Benazir BhuttoPicha: AP

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto, akiwa katika kizuizi cha nyumbani, anashauriana na viongozi wa upinzani dhidi ya rais Pervez Musharraf. Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Pakistan, amezungumza na viongozi wengine tisa wa upinzani wanaompinga rais Musharraf katika siku mbili zilizopita. Hayo ni kwa mujibu wa mpambe wa Benazir Bhutto, Safdar Abbasi.

Wakitafuta kumtenga rais Musharraf baada ya kutangaza hali ya hatari, viongozi wa upinzani wanatumai watafikia makubaliano ya mkutano utakaojumulisha vyama vyote baadaye mwezi huu, ikiwezekana mapema juma lijalo. Mpambe wa Bhutto, Safdar Abbasi, amesema kiongozi huyo anazumguza na viongozi wa vyama vingine vya upinzani na ajenda kubwa ya mazungumzo ni kufufua demokrasia na kurejesha katiba ya mwaka wa 1993.

Katiba hiyo ilisitishwa na rais Musharraf wakati alipotangaza hali ya hatari mnamo Novemba 3. Katika hali hiyo afisa wa jeshi hapaswi kushikilia wadhifa wa kiraia.

Benazir Bhutto amezungumza kwa njia ya simu na kiongozi wa chama cha Jamaat-e-Islami, Qazi Hussain Ahmed, na kumtaka ajiunge na kampeni ya kupigania kurejeshwa demokrasia nchini Pakistan. Bhutto pia amezungumza na kiongozi wa chama cha Tehreek-e- Insaaf, Imran Khan, ambaye anazuiliwa na polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria dhidi ya ugaidi. Khan amekuwa akimkosoa Benazir Bhutto kwa juhudi zake za kugawa madaraka na rais Pervez Musharraf.

Imran Khan ameyakaribisha matamshi ya Benazir Bhutto kwamba chama cha Pakistan People´s Party, PPP, kitaugomea uchaguzi ikiwa utafanyika katika utawala wa hali ya hatari. Bhutto pia juzi Jumanne alimtaka rais Pervez Musharraf ajiuzulu nyadhifa zake za urais na kamanda mkuu wa jeshi la Pakistan.

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan aliye uhamishoni, Nawaz Sharrif, amesema leo kwamba yuko tayari kushirikiana na kiongozi wa upinzani, Benazir Bhutto, kupinga utawala wa kijeshi wa rais Musharraf. Benazir Bhutto amekuwa akijaribu kuunda muungano wa upinzani na amekuwa akizungumza na wanachama wa chama chake Nawaz Sharif.

Benazir Bhutto na Nawaz Sharif wote wawili wameshauriana na kiongozi wa chama cha Awami National Party, Wali Khan, na viongozi wote watatu wamekubaliana kuzindua vita vya pamoja dhidi ya utawala wa hali ya hatari. Nawaz Sharif ambaye anaishi uhamishoni nchini Saudi Arabia, ameukaribisha mwito wa Benazir Bhutto kumtaka rais Pervez Musharraf ajiuzulu. Sharif amesema upinzani unatakiwa uungane dhidi ya mtawala huyo wa kijeshi.

Tofauti iliyopo kati ya rais Musharraf na Benazir Bhutto unaashiria kwamba Bhutto hatoruhusiwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan kwa mara ya tatu. Rais Musharaf amesema Benazir Bhutto tayari amekuwa waziri mkuu mara mbili na kwa mujibu wa sheria haruhusiwi tena kuwa waziri mkuu kwa mara ya tatu. Aidha rais Musharraf amesema itakuwa vigumu kufanya kazi na Bi Bhutto.

Katika makala yake iliyochapishwa na gazeti la New York Times nchini Marekani, Benazir Bhutto, amemkosoa vikali rais Pervez Musharraf akisema yanayoendelea nchini Pakistan ni vurugu tupu. Amesema huku Pakistan ikijiandaa kufanya uchaguzi, shida iliyopo ni kwamba hakuna dalili zozote zinazoonyesha kuwa rais Musharraf atatimiza ahadi yake ya kujiuzulu kama kamanda mkuu wa jeshi hii leo.