1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bibi wa Kifaransa ashikwa mateka Lamu, Kenya

1 Oktoba 2011

Walinzi wa mwambao nchini Kenya wanapambana na wahalifu waliojihami kwa silaha wanaomshikilia mateka bibi mmoja wa Kifaransa.

https://p.dw.com/p/12kMz
Ramani ya Kenya

Taarifa zinaeleza kuwa wahalifu hao wamefyatua risasi angani. Kwa mujibu wa mpenzi wa bibi huyo, John Lepapa, watu sita waliofunika nyuso zao na kujihami kwa silaha, waliwavamia walipokuwa kwenye nyumba yao ya binafsi iliyoko ufuoni mwa bahari kwenye eneo la Manda.

Katika purukushani zote hizo, wahalifu hao walimuamuru bibi huyo wa Kifaransa aliye na umri wa kiaka 66 na mpenzi wake wake pamoja na wasaidizi wa nyumbani kulala kifudifudi kabla ya mmoja wao kumkamata na kumpeleka kwenye mashua iliyokuwa ikisubiri ufuoni.

Flash-Galerie Piraterie Somalia Kenia Polizei
Kitengo cha kupambana na waharamia nchini Kenya kwenye eneo la mpakani na Somalia.Picha: DW

Pindi baada ya tukio hilo, Waziri wa Utalii, Najib Balala, aliyezungumza na shirika la habari la Reuters, alithibitisha kuwa vurumai hizo zinatokea katika eneo linalopakana na Somalia na wahalifu hao wanafyatua risasi angani ili kuwatia hofu watu walio karibu. Kulingana na Waziri Najib Balala, jambo linalotia wasiwasi ni kuwa endapo watalizamisha boti alilomo bibi huyo wa Kifaransa ambaye ni mlemavu, huenda akayapoteza maisha yake. 

Mpenzi wa bibi huyo Lepapa aliye na umri wa miaka 39 amesema bibi huyo wa Kifaransa anaumwa saratani na hana dawa anazozihitaji kwa dharura.

Kenia Piraterie MV York
Meli inayopiga doria kwenye pwani ya KenyaPicha: dapd

Wakati huohuo, Ufaransa imetoa ilani rasmi kuwaonya raia wake kutolizuru eneo la Lamu linalopakana na nchi ya Somalia.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-RTRE,AFPE Mhariri: Mohamed, Dahman