1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden adai Urusi inakusudia kutumia silaha za kemikali

Sylvia Mwehozi
22 Machi 2022

Jeshi la Ukraine limeonya hii leo juu ya mashambulizi zaidi ya makombora ya Urusi dhidi ya miundombinu muhimu wakati rais wa Marekani Joe Biden naye akitoa onyo kali kwamba Moscow inazingatia kutumia silaha za kemikali. 

https://p.dw.com/p/48pOO
Ukraine I Zerstörung in Mariupol
Picha: Sergey Bobok/AFP/Getty Images

Vikosi vya Urusi vimeshindwa kudhibiti mji wowote mkubwa wa Ukraine katika mapigano ya zaidi ya wiki nne tangu kuanza kwa uvamizi wake na kuongeza uharibifu wa maeneo ya makaazi ya raia, mashambulizi ya anga, makombora ya masafa marefu na mizinga.

Mji wa kusini wa Mariupol umekuwa kitovu cha mashambulizi ya Urusi na kwa kiwango kikubwa umeharibiwa huku miili ikizagaa mitaani. Mashambulizi makali pia yameripotiwa katika mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv siku ya Jumatatu.

Kwenye taarifa yake, jeshi la Ukraine limesema kwamba vikosi vya Urusi vinatarajiwa kuendeleza mashambulizi na kulenga miundombinu muhimu kwa kutumia "silaha za hali ya juu na za kemikali".

Rais wa Marekani Joe Biden bila ya kutoa ushahidi alisema madai ya uongo ya Urusi kwamba Ukraine inazo maabara za kibayolojia na silaha za kemikali, yanaashiria kuwa rais Vladimir Putin "yuko katika hali mbaya" na anakusudia kutumia silaha kama hizo.

Wa-Ukraine waapa kutetea maeneo yao

"Tayari ametumia silaha za kemikali hapo awali, na tunapaswa kuwa waangalifu kuhusu kile kitakachokuja. Anajua kutakuwa na matokeo mabaya kwa sababu ya umoja wa NATO, lakini hoja ni ya ukweli".

Biden pia alitoa tahadhari juu ya mashambulizi ya mtandaoni yanayoweza kufanywa na Urusi, akisema hiyo ni sehemu ya mchezo wa Moscow. Urusi kwa upande wake imekana kuwashambulia raia ingawa uharibifu ulioshuhudiwa katika miji ya Mariupol na Kharkiv ni ukumbusho wa mashambulizi ya Urusi katika miji ya huko Chechnya na Syria. Biden anatarajiwa kufanya ziara barani Ulaya wiki hii kukutana na washirika wake ili kujadili vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.

Ukraine I Zerstörung in Mariupol
Moja ya jengo la makaazi ya raia lililoharibiwa mjini MariupolPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/picture alliance

Katika hatua nyingine, vikosi vya Ukraine vimedai kudhibiti tena kitongoji muhimu katika mji mkuu Kyiv mapema leo Jumanne. Wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema katika taarifa yake kwamba majeshi yake yamevifurusha vikosi vya Urusi kutoka kitongoji cha Makariv baada ya mapambano makali. Hatua hiyo imeruhusu vikosi vya Ukraine kuidhibiti tena njia muhimu na kuzuia vikosi vya Urusi kuweza kuzingira mji wa Kyiv kutokea upande wa Kaskazini Magharibi.

Lakini tena wizara hiyo ya ulinzi ikadai kwamba vikosi vya Urusi vinavyopambana kuelekea mjini Kyiv vilifanikiwa kwa kiasi kidogo kudhibiti baadhi ya vitongoji vya Bucha, Hostomel na Irpin ambavyo vimekuwa chini ya mashambulizi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anatarajiwa kulihutubia bunge la Japan kesho Jumatano akitafuta uungwaji mkono zaidi wa kimataifa katika mapambano ya nchi yake dhidi ya Urusi. Japan tofauti na kipindi cha nyuma, imekuwa na msimamo mkali dhidi ya Urusi sambamba na mataifa mengine ya kundi la nchi saba, ingawa hatua za Japan zimezua ulipaji kisasi kutoka kwa Moscow.

Siku ya Jumatatu rais Zelensky alisisitiza rai yake kwa ajili ya mazungumzo ya moja kwa moja na rais wa Urusi Vladimir Putin, akitangaza kwamba yuko tayari kukutana na kiongozi huyo kwa namna yoyote kujadili jinsi ya kumaliza mzozo huo wa karibu mwezi mmoja.