1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Putin asithubutu kutumia silaha za sumu Ukraine

Lilian Mtono
18 Septemba 2022

Rais wa Marekani amesema kama Moscow itatumia silaha za kimbinu za nyuklia, itatengwa hata Zaidi na ulimwengu. Vikosi vya Urusi vinaripotiwa kuilenga Zaidi miundombinu ya kiraia nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/4H1nf
USA US-Präsident Joe Biden spricht im Weißen Haus in Washington über Gaspreise
Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Rais Joe Biden wa Marekani amemuonya mwenzake wa Urusi Vladmir Putin dhidi ya kutumia silaha za sumu au kimbinu baada ya kukumbwa na hasara kubwa katika vita vya Moscow nchini Ukraine.

Soma pia: Zelensky afanya ziara Izium

"Usijaribu. Usijaribu. Usijaribu," ameikiambia kipindi cha televisheni ya Marekani cha "60 Minutes" katika mahojiano yanayorushwa leo Jumapili.

"Utabadilisha sura ya vita hivi na kuwa kitu hakijawahi onekana tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,” amesema Biden. Alipoulizwa jibu la Marekani litakuwa lipi, Biden alisema hatua ya aina hiyo itakuwa na "madhara makubwa.”

Ukraine | Krieg | Massengräber in Izium
Miili ilipatikana katika kaburi la pamoja IziumPicha: Emmanuelle Chaze/DW

"Watatengwa Zaidi ulimwenguni kuliko walivyowahi kuwa wakati mwingine wowote,” amesema rais huyo. "Na kwa kuzingatia kile watakachokifanya kitaamua aina ya jibu litakalotolewa.”

Soma pia: Ukraine yaendelea kurejesha maeneo yaliyodhibitiwa na Urusi

Silaha za kimbinu za nyuklia zinaweza kutumiwa katika masafa mafupi na kwa ujumla huwa ndogo katika nguvu, ijapokuwa vichwa vya kisasa vya kimbinu vya makombora vina nguvu mara kadhaa zaidi ya vilivyotumiwa na Marekani wakati wa Vita Vya Pili vya Dunia mjini Hiroshima na Nagasaki.

Urusi yalenga miundombinu ya raia

Uingereza imesema Urusi imepanua mashambulizi yake kwenye miundombinu ya kiraia nchini Ukraine katika wiki iliyopita na kuna uwezekano wa kupanua wigo zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa raia watano waliuawa katika mashambulizi ya Urusi huko Donetsk, na katika mkoa wa Nikopol majengo ya juu na ya kibinafsi, mabomba ya gesi na nyaya za umeme ziliharibiwa na mashambulizi ya Urusi.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza katika taarifa yake ya karibuni ya kijasusi imesema wakati ikiendelea kupata hasara katika uwanja wa mapambano, inawezekana Urusi imepanua maeneo inayojiandaa kushambulia katika jaribio la kuhujumu moja kwa moja morali wa watu wa Ukraine na serikali yake.

Scholz amrai Putin kutafuta suluhisho la kidiplomasia

Zelenskyy aituhumu Urusi kwa mbinu za Kinazi 

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema uchunguzi umegundua Ushahidi wa maeneo kumi ya kufanyia vitendo vya mateso katika miji iliyokombolewa kaskazini mashariki ya jimbo la Kharkiv.

"Mateso ni mbinu iliyotumiwa sana katika maeneo yaliyokaliwa. Hicho ndicho Manazi walikifanya – hiki ndicho Warusi wanafanya,” alisema Zelensky katika hotuba yake ya video Jumamosi usiku. "Watajibu katika njia ile ile – kwenye uwanja wa mapambano na kwenye vyumba vya mahakama;” aliapa.

Mapema wiki hii, Zelensky alisema Zaidi ya miili 400 iligundulika katikakaburi la Pamoja katika mji wa Izium mkoani Kharkiv baada ya wanajeshi wa Ukraine kuukomboa kama sehemu ya operesheni ya kuyakamata maeneo yaliyo mikononi mwa Moscow.

Afp, reuters, dpa, ap