1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden: Nimechukizwa na shambulio la hospitali Gaza

18 Oktoba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amewasili mjini Tel Aviv leo huku hasira za raia wa Mashariki ya Kati zikizidi kufuatia mauaji ya mamia ya watu katika hospitali mjini Gaza.

https://p.dw.com/p/4XgQt
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanjahuPicha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Rais Joe Biden ameeleza uungwaji mkono usioyumba kwa Israel katika vita vyake dhidi ya Hamas kuhusiana na mashambulizi ya kundi hilo ya Oktoba 7, na amekaribishwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Lakini tukio la vifo vya hospitali limetishia kuvuruga ziara yake hiyo, huku Jordan ikifuta mkutano wa kilele ambapo Mfalme Abdullah II alitarajiwa kumualika Biden, Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas, na Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi.

Kundi la Hamas limesema shambulio la Israel ndiyo liliharibu hospitali ya Gaza, huku Israel ikisema roketi lililofyatuliwa vibaya na kundi la Islamic Jihadi ndiyo liliipiga hospitali hiyo ya Ahli Arab, ambapo watu kati ya 200 na 300 wameripotiwa kuuawa, kulingana na maafisa wa afya wa Gaza. Ingawa Hamas imetaja vifo zaidi ya 500.

Soma pia:Hamas na Israel zalaumiana kwa shambulio la hospitali Gaza

Muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Biden, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari aliuambia mkutano wa habari kwamba ushahidi walio nao unathibitisha kuwa mlipuko wa hospitali hiyo ulisababishwa na roketi lililofyatuliwa na Islamic Jihad.

Akizungumza na Netanyahu, Rais Biden amemuambia waziri mkuu huyo wa Israel kuwa kulingana na alichokiona, shambulio hilo linaonekana lilifanywa na kile alichokitaja kuwa timu nyingine, huku akiilaumu Hamas kwa matatizo ya Wapalestina.

Lakini Biden amesema kuna watu wengi duniani ambao hawana uhakika juu ya nini kilisababisha mlipuko huo, ambao amesema umemhuzunisha na kumkasirisha.

Shambulio lazusha hasira mashariki ya kati

Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi amesema Wamisri watakataa uhamishaji wa lazima wa mamilioni ya Wapalestina kuwapeleka rasi ya Sinai, na kuongeza kuwa hatua kama hiyo itaigeuza rasi hiyo kuwa kituo cha mashambulizi dhidi ya Israel.

Ägypten | Präsident Abd al-Fattah as-Sisi
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi Picha: Ahmad Hassan/AFP/Getty Images

Sissi amesema katika mkutano wa pamoja na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Cairo, kwamba Ukanda wa Gaza uko katika udhibiti kamili wa Israel na badala yake Wapalestina wanaweza kupelekwa katika jangwa la Negev hadi wapiganaji wa Hamas watakaposhughulikiwa. 

Kwa upande wake Kansela Scholz amerudia kulaanimashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel na kutoa wito wa msaada wa kibinadamu kuruhusiwa kuwafikia watu wa Gaza.

Kwa pamoja tunashughulikia njia za kibinadamu kwa Gaza haraka iwezekanavyo. Watu huko wanahitaji maji, chakula na dawa. Ninaweza kuwahakikishia kwa wakati huu hatutawaacha watu hao peke yao.

Serikali ya Shirikisho itaendeleza juhudi zake za kibinadamu kwa Gaza ili kupunguza mateso ya raia.

Soma pia:Biden adai ameghadhabishwa na mashambulizi hospitali Gaza

Mashambulizi ya hospitali ya Gaza yamezusha hasira kote Mashariki ya Kati, hata wakati Biden akijaribu kutuliza hali na kuzuwia mzozo huo kusambaa nje ya mipaka.

Vikosi vya usalama vya Palestina vilifyatua gesi ya kutoa machozi na magruneti ya kupoteza fahamu kuwatawanya waandamanaji mjini Ramallah, ambao ndiyo makao makuu ya rais wa Palestina Mahmoud Abbas, mmoja wa viongozi wa Kiarabu waliofuta mkutano na Biden.

Maandamano pia yamefanyika kwenye balozi za Israel nchini Uturuki na Jordan, na karibu na Ubalozi wa Marekani nchini Lebanon, ambako vikosi vya usalama vilifyatua gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollah, amelitolea wito shirika la ushirikiano wa mataifa ya Kiislamu OIC, kuiwekea vikwazo Israel na kutekeleza marufuku ya mafuta dhidi ya taifa hilo, pamoja na kuwafukuza mabalozi wake.
 

Watu zaidi ya 500 wadaiwa kuuwawa hospitalini Gaza