1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter aangazia macho muhula mwingine kama rais wa FIFA

9 Mei 2014

Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni - FIFA Sepp Blatter, amedokeza kwamba anapanga kugombea tena kama rais kwa muhula wa tano akidai kuwa bado hajakamilisha majukumu yake

https://p.dw.com/p/1BxFF
Sepp Blatter
Picha: picture-alliance/dpa

Blatter amenukuliwa na gazeti moja nchini Uswisi akisema kuwa angependa kugombea, kwa sababu kazi bado haijakamilika. Blatter mwenye umri wa miaka 78 amesema mamlaka yake yanafikia ukingoni, lakini jukumu lake halijakamilika.

Mswisi huyo amekuwa katika uongozi wa FIFA tangu mwaka wa 1998. Uamuzi wake wa kuashiria kuwa atagombea, unakuja zikiwa zimesalia wiki chache tu kabla ya kung'oa nanga dimba la Kombe la Dunia nchini Brazil Juni 12. Uchaguzi huo utaandaliwa mwaka wa 2015.

Mgombea pekee ambaye amejitosa rasmi katika kinyang'anyiro hicho ni Jerome Champagne, katibu mkuu wa zamani wa FIFA, aliyestaafu mwaka wa 2010. Macho hata hivyo yataangaziwa rais wa Shirikisho la Soka Ulaya – UEFA Michel Platini ambaye alidai kuwa yeye ndio mtu pekee anayeweza kumpiku Blatter katika uchaguzi. Lakini Mfaransa huyo hajafanya uamuzi kama atagombea akisisitiza kuwa atatoa msimamo wake baada ya Kombe la Dunia.

Maandalizi ya viwanja vitakavyoandaa mechi za dimba la kombe la Dunia Brazil yanaelekea kukamilika
Maandalizi ya viwanja vitakavyoandaa mechi za dimba la kombe la Dunia Brazil yanaelekea kukamilikaPicha: picture-alliance/dpa

Waakti huo huo Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA linaamini kuwa Brazil itakuwa tayari kuandaa dimba la Kombe la Dunia mwezi ujao wakati ikiharakisha kumalizia kwa wakati unaofaa ujenzi wa viwanja vyote 12.

Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke amesema kila kitu hakijakamilika kwa kinyang'anyiro hicho kinachong'oa nanga Juni 12 hadi Julai 13. Siku ya Alhamis, Polisi nchini Brazil walifanya mgomo wa saa 24 wakidai mazingira bora ya utendaji kazi, ikiwa ni siku 37 pekee kabla ya nchi hiyo kuandaa dimba la Kombe la Dunia. Polisi imetishia tena kugoma wakati wa tamasha hilo la soka la kimataifa. Polisi waligoma katika miji kadhaa itakayoandaa Kombe la Dunia pamoja na mji mkuu Rio, ambao utaandaa mechi saba ikiwemo fainali ya dimba hilo mnamo Julai 13.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu