1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter kujiuzulu kama rais wa FIFA

3 Juni 2015

Safari ya Sepp Blatter imefikia kikomo kwa ghafla, siku chache tu baada ya kuonekana kuimarisha udhibiti wake katika shirikisho la kandanda ulimwenguni – FIFA

https://p.dw.com/p/1FavH
FIFA - Präsident Blatter tritt zurück
Picha: VALERIANO DI DOMENICO/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo wa mchezo maarufu zaidi ulimwenguni, mwenye umri wa miaka 79 alipuuza hasira ya ulimwengu wiki iliyopita na kushinda muhula mwingine wa miaka minne ofisini. Lakini kuchaguliwa kwake tena kuliongeza shinikizo kutoka kwa wenzake, wadhamini, wanamichezo na mashabiki waliomtaka ajiuzulu kama rais wa FIFA.

Katika kikao cha waandishi wa habari kilichoandaliwa ghafla hapo jana jioni, Blatter alitangaza kuwa ataondoka usukani katika miezi michache ijayo na akaitisha uchaguzi mpya wa kumchagua mrithi wake. "nimezingatia kwa kina wadhifa wangu wa urais na miaka 40 iliyopita ya maisha yangu ambayo yamehusiana kwa karibu na FIFA na mchezo huu mzuri wa kandanda. Nashukuru na naipenda FIFA zaidi ya kingine chochote na nataka tu kufanya mema kwa kandanda na FIFA na taasisi yetu".

FIFA - Präsident Blatter tritt zurück
Blatter baada ya kutangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wakePicha: VALERIANO DI DOMENICO/AFP/Getty Images

Tangazo hilo la Blatter limeiacha FIFA bila kiongozi na bila mkondo wa wazi wa kuendelea mbele. Limezusha mapambano ya kimataifa ya madaraka ya udhibiti wa shirikisho hilo wakati uchunguzi wa uhalifu dhidi ya maafisa wake wakuu akiwemo Blatter mwenyewe ukipamba moto.

Blatter aliyeonekana kuwa mchovu, aliisoma taarifa hiyo ya dakika sita katika lugha ya Kifaransa kabla ya kuondoka bila kujibu maswali yoyote. Mswisi huyo alipata kura 133 dhidi ya 73 za mpinzani wake Mwanamfalme Ali bin al-Hussein wa Jordan lakini hayo yote ni kama yamesahaulika "japokuwa wanachama wa FIFA wamenichagua tena kama rais, jukumu hili halionekani kuungwa mkono na kila mtu katika ulimwengu wa kandanda, mashabiki, vilabu, wachezaji, wale wanaohamasisha maisha katika kandanda, kama tu tunavyofanya katika FIFA. Ndio maana nitaitisha mkutano maalumu wa wanachama na kujiuzulu wadhifa wangu. Utaandaliwa haraka iwezekanavyo na rais mpya atachaguliwa kuchukua nafasi yangu. Nitaendelea kuhudumu kama rais wa FIFA hadi uchaguzi mpya utakapoandaliwa".

FIFA Rücktritt Blatter Domenico Scala
Mwenyekiti wa kamati ya ukaguzi ya FIFA Domenico Scala asema Imani inastahili kurejeshwaPicha: picture-alliance/dpa/E. Leanza

Uchaguzi unatarajiwa kuandaliwa kati ya Desemba na Machi mwaka ujao. Mwanamfalme Ali bin al Hussein wa Jordan amekataa kusema ikiwa atagombea tena.

Michel Platini, rais wa Shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA, alitoa wito kwa Blatter kujiuzulu wiki iliyopita kabla ya uchaguzi. Na hapo jana ameusifu uamuzi wa Blatter kung'atuka. Amesema ni uamuzi mgumu na wa ujasiri na uliostahili. Platini alimuunga mkono Mwanamfalme Ali katika uchaguzi wa wiki iliyopita lakini sasa kiungo huyo wa zamani wa Ufaransa na Juventus anawezekana kuwa mgombea katika uchaguzi ujao.

Athari za kura za kutolewa vibali vya kuandaliwa Kombe la Dunia zilizopigwa Desemba 2010 ziliugubika muhula wa mwisho wa Blatter madarakani, na rais mpya huenda akataka kuyatathmini upya maamuzi hayo.

Blatter amesema FIFA inastahili mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuwekwa kikomo cha mihula ili kuhakikisha kuwa katika siku za usoni rais wa FIFA anazingatia muda wake madarakani. Kamati kuu ya FIFA ambayo pia ilizichagua Urusi na Qatar kuandaa kombe la Dunia 2018 na 2022 pia inakabiliwa na mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kikomo cha muhula, wanachama wachache na uchunguzi mkali wa uadilifu utakaowekwa na FIFA.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri:Josephat Charo