1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter na wenzake walijilipa dola milioni 80

4 Juni 2016

Shirika la Kimataifa la Kandanda - FIFA limesema kuwa rais wake wa Zamani Sepp Blatter na wasaidizi wake wawili walijizawadia zaidi ya dola milioni 80 katika malipo yanayotiliwa shaka katika kipindi cha miaka mitano

https://p.dw.com/p/1J0ai
Zürich FIFA Kongress Blatter und Valcke
Picha: Reuters/R. Sprich

Wapelelezi wa Uswisi walifanya upekuzi katika makao makuu ya FIFA wakati shirikisho hilo la kandanda la kimataifa lilifuchua kuwa rais wake wa zamani Sepp Blatter na wasaidizi wake wawili walijizawadia zaidi ya dola milioni 80 katika malipo yanayotiliwa shaka katika kipindi cha miaka mitano.

Katika siku ambayo pia FIFA ilikanusha ripoti za vyombo vya habari kuwa rais mpya Gianni Infantino anafanyiwa uchunguzi, ilisema Blatter katibu mkuu wa zamani Jerome Valcke na mkurugenzi wa fedha Markus Kattner walifanya juhudi zilizopangwa “kujinufaisha”.

Blatter anatumikia adhabu ya kufungiwa miaka sita kujishughulisha na kandanda kuhusiana na malipo ya dola milioni mbili yaliyotolewa kwa aliyekuwa makamu wa rais wa FIFA Michel Platini. Valcke na Kattner wote walitimuliwa katika miezi ya karibuni kuhusiana na kashfa za tiketi za Kombe la Dunia na malipo waliyopokea.

Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Uswisi imesema wapelelezi wake “walifanya upekuzi katika makao makuu ya FIFA” siku ya Alhamisi kama sehemu ya uchunguzi wake kuhusu usimamizi wa FIFA na kutolewa vibali vya kuandaa vinang'anyiro vya Kombe la Dunia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu