1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Blue card" kuingia Umoja wa Ulaya

Maja Dreyer23 Oktoba 2007

Ukitaka kufanya kazi nchi Marekani inabidi kuombe ruhusa maalum inayojulikana kama “Green Card”, ama kadi ya kijani. Umoja wa Ulaya leo hii umetambulisha mpanga wa kuanzisha mkakati mpya kwa wafanyakazi kutoka nchi za nje ambao utafanana kidogo na “Green Card” wa Marekani. Jina lake lakini ni “Blue Card”, ama kadi ya buluu.

https://p.dw.com/p/C7gT
Nchi za Ulaya zinahitaji wataalamu kutoka nje
Nchi za Ulaya zinahitaji wataalamu kutoka njePicha: AP

Mara kwa mara sekta za kitaaluma za bara la Ulaya, hususan ile ya kompyuta, zinalaumu kwamba zinakosa wataalum. Kamishna wa mambo ya ndani na ya sheria wa Umoja wa Ulaya, Bw. Franco Frattini, ana takwimu nyingine zinazoonyesha tatizo lililoko, kwani asilimia 85 ya wahamiaji wote duniani ambao hawana elimu wanakimbia Ulaya, lakini asilimia 5 ya wale wenye elimu ya juu wanaokuja Ulaya. Kinyume chake huko Marekani ambapo asilimia 55 ya wasomi wanakimbilia huko pamoja na asilimia 5 ya wasio na elimu.

Mradi wa “Blue Card” basi unalenga kuwavutia wasomi na wataalamu kwa kurahisisha masharti ya uhamiaji, anaeleza kamishna Franco Frattini: “Kwa njia hiyo, Ulaya inatelekeza sera za uhamiaji ambazo zinawavutia wale wanaohitajika kwenye soko la ajira barani humu.”

Kadi hiyo ya buluu inatakiwa kushindana na “Green Card” ya Marekani ambayo inatoa ruhusa ya kufanya kazi Marekani bila ya kuweka muda. “Blue Card” ya Ulaya lakini kwanza ni ruhusa kwa miaka miwili tu na vilevile kuna masharti kadhaa. Kwanza inabidi msharaha wa mhamiaji mtaalamu uwe mkubwa kuliko mishahara ya chini barani Ulaya. Pia inabidi awe na mkataba wa ajira kabla ya kuwasili Ulaya. Baada ya miaka kadhaa huenda atapata ruhusa ya kukaa kabisa. Kwa upande mwingine, kamishna Frattini anataka kurahisisha na kuharakisha utaratibu wa kutoa ruhusa kwa wataalamu. Sheria hiyo mpya lakini haitaweka viwango vya uhamiaji kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, alisema Bw. Frattini. Ni juu ya kila nchi yenyewe kuamua inahitaji wataalamu wangapi kutoka nje.

Lengo lakini ni kusawazisha sheria za uhamiaji katika nchi zote 27 wanachama ambazo zinatofautiana sana ili zielekewe bora zaidi. Juu ya hayo, wataalamu wanaokuja Ulaya watawezeshwa kusafiri katika nchi wanachama na kufanya kazi hapa na pale baada ya miaka michache. Kamishna Franco Frattini: “Mwajiriwa mtaalamu aliyekubaliwa katika nchi fulani, baada ya muda fulani ataruhusiwa kuhamia nchi nyingine ya Ulaya ambapo amepata ajira. Hayo yote ataweza kufanya bila ya kujaza fomu nyingine.”

Kwa mujibu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya uwezo huu wa kufanya kazi katika nchi zote za Umoja huu ni muhimu sana ili kuonyesha faida ya mradi wa pamoja kuliko kila nchi kuwa na sheria zake. Kwa njia hiyo, Umoja wa Ulaya utaweza kuwavutia wataalamu wengi kuliko kila nchi peke yake.

Waziri wa ajira wa Ujerumani, Franz Müntefering, alipinga pendekezo la kamishna huyu wa Umoja wa Ulaya akisema kwamba sheria za uhamiaji ni chini ya mamlaka ya mabunge na serikali za kitaifa. Kamishna Franco Frattini lakini kwa kupendekeza mradi wa “Blue Card” anafuata amri ya halmashauri ya viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya waliomtaka afikirie sera mpya za uhamiaji kwa Umoja wa Ulaya kwa jumla.