1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BoB 2012: Blogu ya Kiirani yashinda

2 Mei 2012

Blogu inayoitwa "Dirisha la Hofu" ya mwanamblogu wa Kiirani, Arash Sigarchi, imechaguliwa mshindi wa blogu bora kwa mwaka huu wa 2012 katika hafla ya uteuzi huo iliyofanyika mjini Berlin kwenye ofisi za Deutsche Welle.

https://p.dw.com/p/14nx8
Mshindi wa Blogu Bora, Arash Sigarchi.
Mshindi wa Blogu Bora, Arash Sigarchi.Picha: privat

Kwa hakika "Dirisha la Hofu" linavitonesha vidonda vya Iran, lakini Arash Sigarchi anaweza kuyafanya hayo  kutokea nje ya  Iran. Katika blogu yake, Sigarschi  anasema "ni kashfa kubwa" ni "fedheha mara mbili" kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Anapigia mfano wa mkasa wa afisa wa kidiplomasia wa ngazi za juu wa Iran aliyemnyanyasa kingono mtoto wa kiume nchini Brazil. Taarifa juu ya kashfa hiyo ilichapishwa kwa kina katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, lakini ubalozi wa Iran ulijaribu kuzipuuza taarifa hizo na kusema kuwa ni matokeo ya kutoelewana kitamaduni. Taarifa kama hizo hazichapishwi katika vyombo vya habari vya Iran au hata vikichapishwa, zinapotoshwa.

Sigarchi anasema utawala wa  Iran unajifanya kuwa na uadilifu wa kuyafuata maagizo ya dini, ambapo kwa utawala huo uhusiano wa mapenzi nje ya ndoa, yaani  zinaa, ni dhambi. Lakini sasa limeripuka bomu dhidi ya utawala huo kwani mwakilishi wake wa kibalozi amemnyanyasa kingono mtoto mdogo wa kiume. Adhabu ya udhalimu huo ni kifungo cha miaka 14  jela.

Yasiyofanywa Iran, yafanywa kwenye "Dirisha la Hofu"

Wakati vyombo rasmi vya Iran havichapishi taarifa kama hizo, blogu ya "Dirisha  la  Hofu"  aliyoianzisha Sigarchi mnamo mwaka wa  2008 akiwa ukimbizini mjini Washington inafanya hivyo.

Jopo la Majaji wa Blogu Bora, BoB, lililofanya uteuzi mjini Berlin.
Jopo la Majaji wa Blogu Bora, BoB, lililofanya uteuzi mjini Berlin.Picha: DW/Tobias Kleinod

Miaka minne kabla ya hapo, wakati bado angali nchini  Iran, Sigarchi alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kuandika maneno ya kukosoa kama  mwandishi. Hata hivyo kutokana na  bidii ya wakili wake, Shirin Ebadi mshindi  wa nishani  ya amani  ya Nobel, adhabu ya Sigarchi ilipunguzwa hadi miaka mitatu.

Lakini baada ya hapo mwandishi habari huyo alianza kuandamwa na mikosi. Ndugu yake Ashkan alikufa katika ajali ya gari. Yeye mwenyewe alipata maradhi ya saratani  wakati  akiwa kifungoni. Lakini hakushika tama.

Miongoni mwa waliokuwamo kwenye jopo la majaji ya Blogu Bora, Arash Abadpour, ambaye pia anatoka Iran, amesema kuwa Sigarchi hakupoteza dira na licha ya mikosi iliyomwandama, mwandishi huyo ameendelea kuwa imara.

Wapinzani wengine wa utawala wa Iran wamedai kwamba Sigarchi anaandika taarifa  zenye mwelekeo wa kuiridhisha serikali, lakini Sigarchi anatumia hoja, akisema kuwa yeye  ni mwandishi wa habari na anachokiandika kina uzito kwa  mtazamo wa  kiuandishi.

Mwandishi huyo alichaguliwa na  jopo la kimataifa la waamuzi 12  kwenye  makao ya Deutsche Welle jijini Berlin. Mhariri Mkuu wa Deustche Welle, Ute Schaeffer, amesema DW ni  Umoja  wa Mataifa wa Blogu na miradi ya tovuti

Ute  Schaeffer amesema Deutsche Welle imejenga jina zuri duniani kote kutokana na kuandaa mashindano haya ya Blogu Bora.

Mwandishi: Aya Bach
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman