1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram wakabiliwa na Chad

Mjahida4 Februari 2015

Wanajeshi wa Chad, wametangaza kuudhibiti mji wa Gamboru uliokuwa umetekwa na wanamgambo wa Boko Haraam, saa chache baada ya kuanzisha shambulio la ardhini dhidi ya wanamgambo hao

https://p.dw.com/p/1EVKe
Baadhi ya wanajeshi wa Chad
Baadhi ya wanajeshi wa ChadPicha: AFP/Getty Images/M. Medina

Takriban wanajeshi 2000 wa Chad waliokuwa na magari ya kivita walivuka mpaka na kuingia mjini Gamboru nchini Nigeria kutoka mji wa Cameroon wa Fokotol baada ya siku kadhaa za mapigano na wanamgambo wa Boko Haram.

Kulingana na muandishi habari wa shirika la AFP, jana jioni wanajeshi wa Chad walifanikiwa kuchukua udhibiti wa mji huo kutoka kwa wanamgambo wa Boko Haram. Muandishi huyo amesema nyumba kadhaa ziliharibiwa pamoja na maduka huku wakaazi na wanamgambo wakiukimbia mji huo.

Mpaka sasa hakuna idadi kamili ya idadi ya vifo vilivyotokana na shambulio hilo, lakini mwanajeshi mmoja wa Chad amesema wanajeshi wanane waliuwawa huku wengine 20 wakijeruhiwa katika shambulio hilo.

"Tumeliondoa hili kundi la kigaidi," alisema kamanda wa kijeshi wa Chad aliyeongoza operesheni hiyo Ahmat Dari huku akiahidi kupambana na kundi hilo hadi mwisho wake.

Moja ya mashambulizi yanayoaminika kufanywa na Boko Haram, Nigeria
Moja ya mashambulizi yanayoaminika kufanywa na Boko Haram, NigeriaPicha: Reuters

Hatua ya jeshi la Chad imekuja baada ya viongozi wa Umoja wa Afrika wiki iliyopita, kuunga mkono kuundwa kwa kikosi cha wanajeshi 7,500 kutoka nchi tano za Afrika Magharibi kupambana na kitisho cha kusambaa kwa kundi hilo.

Nigeria imekosolewa kushindwa kulidhibiti kundi la Boko Haram

Nigeria imekuwa ikikosolewa, kushindwa kulidhibiti kundi la Boko Haram lililozidisha mashambulizi Kaskazini mwa nchi hiyo wakati ikijitayarisha kwa uchaguzi wa Urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi wa Februari.

Hata hivyo hatua ya jeshi la Chad kujiunga na mapambano dhidi ya Boko Haram inaonyesha wazi, juhudi zinazofanywa na nchi jirani na Nigeria kuzuwiya mipaka yao isiingiliwe na kundi hilo la kigaidi.

Kwa upande mwengine siku ya Jumatatu Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria anayewania kipindi kingine cha urais nchini humo anayeshindana na mgombea mwengine aliyeahidi kupambana vikali na kundi hilo, alinusurika shambulio la kujitoa muhanga lililofanywa na Boko Haram katika eneo la Gombe alikokuwa akifanyia kampeni zake.

Huku hayo yakiarifiwa wanajeshi wa Cameroon wameripotiwa kukabiliana vikali na wanamgambo wa Boko Haram hii leo asubuhi katika mji wa Fokotol unaopakana na Nigeria.

Afisa mmoja wa usalama amesema wanamgambo hao walijaribu kuingia katika mji huo baada ya kufurushwa mjini Gamboru lakini amesema wanajeshi wake bado wanapambana na kundi hilo.

Wakati huo huo baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi yanayofanywa na kundi hilo la kigaidi na kuhimiza ushirikiano wa kijeshi wa serikali za nchi jirani na Nigeria katika kulidhibiti kundi hilo linalohatarisha usalama wa Afrika Magharibi na Afrika ya kati kwa ujumla.

Mwandishi Amina Abubakar AFP/AP

Mhariri Josephat Charo