1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Ugaidi

Boko Haram yaua wanajeshi 150 wa Chad na Nigeria

Mohammed Khelef
25 Machi 2020

Mashirika ya habari ya Reuters na AP yanaripoti kuwa kundi la kigaidi la Boko Haram limewauwa takribani wanajeshi 150 katika mataifa ya Chad na Nigeria ndani ya kipindi cha siku tano zilizopita.

https://p.dw.com/p/3a19Q
Mali - Französische und malische Truppen töten in Mali 30 Dschihadisten
Picha: Getty Images/AFP/P. Guyot

Kwa mujibu wa Rais Idriss Deby wa Chad, wanamgambo hao wa Boko Haram waliwauwa wanajeshi 92 wa nchi yake na kuwajeruhi wengine 47 katika mashambulizi mabaya kabisa dhidi ya jeshi siku ya Jumatatu.

Taarifa ya Rais Deby ilitolewa Jumanne jioni, wakati kiongozi huyo ambaye mwenyewe ni mwanajeshi alipotembelea kisiwa cha Boma kwenye Ziwa Chad, magharibi mwa nchi hiyo, ambako mashambulizi hayo yalifanyika.

Muungano wa kijeshi wa mataifa ya Chad, Niger na Nigeria umeweka kambi yake huko kupambana na uasi wa Boko Haram, ambao umesambaa kwenye mataifa kadhaa ya magharibi mwa Afrika na Ukanda wa Sahel.

"Nimewahi kushiriki kwenye operesheni kadhaa za kijeshi, lakini haijawahi kutokea kwenye historia yetu kupoteza wanajeshi wengi kama hawa kwa wakati mmoja,” Deby aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne.

Frankreich G5-Sahel Gipfel in Pau
Rais wa Chad Idriss Deby.Picha: DW/F. Tiassou

Picha za televisheni ya taifa zilimuonesha Deby, ambaye ameitawala Chad tangu mwaka 1990 na kunusurika kwenye majaribio kadhaa ya mapinduzi na uasi, akitembea kwenye mabaki ya magari yaliyochomwa moto.

Tukio la "bahati mbaya"

Huko kaskazini mwa Nigeria nako, wanamgambo wa Boko Haram wanaripotiwa kuwauwa wanajeshi wengine 50 wa Nigeria katika jimbo la Yobe, kwa mujibu wa duru za kijeshi.

Msemaji wa jeshi la Nigeria, Meja Jenerali John Enenche, aliliambia shirika la habari la AP siku yaJumanne kwamba jeshi lake limepoteza watu wengi katika kile alichokiita "bahati mbaya”, ingawa alikataa kutaja idadi kamili ya wanajeshi waliouawa.

Jeshi hilo lilivamiwa wakati likijiandaa na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Boko Haram, kwa mujibu wa afisa mwengine wa ngazi za juu wa jeshi, ambaye anafahamu operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa afisa huyo, wanajeshi walikabiliana na wanamgambo hao kwa muda mchache, lakini baadaye walilaazimika kukimbia kunusuru maisha yao, kabla ya kurejea tena kupambana na kushambuliwa kwenye kijiji kimoja kiitwacho Gorge.

Tschad Armee Soldaten Zeremonie
Baadhi ya wanajeshi wa Chad wakiwa katika operesheni ya luteka za kijeshi.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Wapiganaji wa Boko Haram walitumia makombora na bunduki kwenye mashambulizi hayo. Manusura na majeruhi wanaendelea kutibiwa kwenye hospitali za Damaturu na Maiduguri.

Wakati Boko Haram ikionekana kuja juu upya baada ya kipindi kirefu cha kuzidiwa nguvu na muungano wa kijeshi, kwenye mataifa mengine ya ukanda huo – Mali, Burkina Faso na magharibi mwa Niger – kundi linalowaunganisha wafuasi wa Al-Qaida na wale wajiitao Dola la Kiislamu linaimarisha nguvu zake na tayari limeshauwa mamia ya wanajeshi ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita.

Uasi wa Boko Haram, ambao ulianza kaskazini mashariki mwa Nigeria mwaka 2009, umeshaangamiza maisha ya watu zaidi ya 30,000 na kuwalazimisha wengine wapatao milioni mbili kuyakimbia makaazi yao.


Chanzo: AP/Reuters