1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram yazidi kuhangaisha Nigeria

9 Januari 2015

Mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria huenda yameua mamia ya watu katika takriban maeneo 11,kwa mujibu wa taarifa za maafisa nchini humo

https://p.dw.com/p/1EHoD
Picha: Reuters

Taarifa zinasema idadi kamili ya waliuwawa hadi sasa haijafahamika ingawa vijiji 11 vimeteketezwa kwa moto. Matukio hayo yanazidi kukemewa na Jumuiya ya Kimataifa huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akitowa mwito wa kibinafsi wa kulitaka kundi hilo kuwaachia mamia ya watoto waliowateka nyara mwaka uliopita.

Mashambulio yaliyotokea siku ya jumatano yamesababisha taharuki zaidi nchini Nigeria huku taarifa zilizotolewa na mkuu wa mji wa baga ulioko katikati ya vijiji 11 vilivyoshambuliwa akisema idadi ya waliouwawa huenda ikawa ni mamia ya watz.Hata hivyo maafisa wote waliozungumzia kuhusu mashambulizi haya wamezipinga taarifa zinazodai kwamba waliouwawa wanafikia watu 2000.

Wanajeshi wakipiga doria katika mpaka na Cameroon
Wanajeshi wakipiga doria katika mpaka na CameroonPicha: Getty Images/Afp/Reinnier Kaze

Afisa mmoja wa usalama anayeihsi katika jimbo la Borno anasema wengi wa watu kutoka vijiji hivyo wamekimbilia vichakani kuokoa maisha yao. Juu ya hilo mkuu wa mji wa Baga aliyezungumza na vyombo vya habari amearifu kwamba idadi kubwa ya wahanga wa mashambulizi hayo huenda ni ya watu kutoka mji huo kwakuwa ni mji wenye idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na idadi ya wanaoishi vijijini.

Aidha inatajwa kwamba hali ya mawasiliano ya simu sio nzuri na ndio sababu hadi sasa imekuwa vigumu kupatikana kwa taarifa za kuthibitika ingawa serikali imeanza kupeleka msaada kwenye eneo hilo. Kundi la Boko haram limesemekana kushambulia eneo hilo la Baga siku kadhaa zilizopita kabla ya mashambulio haya ya Jumatano na kuiteka pia kambi ya kijeshi hali iliyowafanya wakaazi wa eneo hilo kukimbilia nchini Chad huku mamia ya wengine wakiwa wameuwawa.

Kutokana na kuzidi kwa matukio ya mashambulizi Jumuiya ya Kimataifa inapaaza sauti kulaani mauaji yanayofanywa na kundi hilo la Boko Haram.Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akizungumza hapo jana katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa alitowa mwito wa kibinafsi kwa kundi hilo kuacha umwagaji damu na kuwaachia huru watoto wanaowashikilia mateka.

Rais Goodluck Ebele Jonathan
Rais Goodluck Ebele JonathanPicha: imago/Wolf P. Prange

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kwa upande wake ameelezea kutamaushwa kwake juu ya mashambulizi hayo ya kaskazini mwa Nigeria.Maelfu ya watu wameuwawa na kundi la Boko Haram mwaka huu pekee.Hapo jana rais Paul Biya ya Cameroon aliiitaka Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati na kusaidia kulimaliza kundi la Boko haram ikiwa ni siku moja baada ya wanamgambo hao kutishia kuongeza mashambulizi nchini Cameroon.Wakati Jana Rais Goodluck Jonathan akizundua rasmi harakati zake za kuwania kuchaguliwa tena maswali mengi yamejitokeza kuhusu vipi Nigeria itakavyoweza kuendesha uchaguzi mnamo Feb 14 hasa katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki ambako kundi la Boko Haram linadhibiti.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessnga