1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolt: ninaendelea kufanya mazoezi makali

24 Julai 2015

Katika riadha sasa na Usain Bolt anasema amekuwa akifanya kila liwezekanalo kupona jeraha lake na anatarajia kufanya vyema katika mashindano ya ubingwa wa Ulimwengu mjini Beijing mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/1G4Lf
Usain Bolt
Picha: Reuters/M. Kappeler

Mwanariadha huyo Mjamaica bingwa wa Olimpiki na Ulimwengu katika mbio fupi na anayeshikililia rekodi pia anasema kuwa anakasirishwa sana na matukio ya wanariadha kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni, lakini yeye siyo ‘mwokozi' wa mchezo wa riadha.

Baada ya msimu wa 2014 uliokumbwa na majeraha na matatizo ya nyonga mwaka huu, Bolt amekimbia mara tano msimu huu, mara moja tu katika mbio za mita 100, wakati alipotumia sekunde 10.12 nchini Brazil mwezi Aprili.

Bolt mwenye umri wa miaka 28 ambaye anashikilia rekodi ya ulimwengu ya sekunde 9.18 katika mita 100 na sekunde 19.19 katika mita 200, atalenga kuyatetea mataji yake katika mashindano ya ubingwa wa dunia mjini Beijing kuanzia Agosti 22. "Kwangu mimi, sina wasiwasi kuhusu muda unaowekwa na wanariadha. Ninajiandaa tu kufanya kila kitu vizuri kwa sababu kila mmoja anafahamu kuwa wakati mwingine mimi huyumba. Hivyo najiandaa kabisa na kuhakikisha kila kitu kiko sawa lakini nina uhakika nitakaposhiriki mashindanoni, kawaida ntakuwa tayari hivyo natarajia kuwa na matokeo bora".

Leichtathletik WM Moskau Mo Farah
Mwanariadha wa Uingereza Mo FarahPicha: Reuters

Wakati huo huo, mwanariadha wa Uingereza Mo Farah anasema tuhuma zinazomkabili kocha wake za matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini hazimwongezei shinikizo lolote la ziada. Kocha Alberto Salazar anatuhumiwa kuhusika na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku madai ambayo anakanusha na Farah anasema suala hilo halimwathiri

"haliniathiri kabisa. Ni shinikizo tu unalojiwekea mwenyewe. Lakini unajua kila siku naamna asubuhi na kufurahia ninachokifanya mradi ninashinda medali nyingi na kuiwakilisha nchi yangu na hicho ndicho kinachonipa motisha zaidi.

Bingwa huyo wa Olimpiki, Ulimwengu na Ulaya katika mbio za mita 5,000 na 10,000 ananuia kutetea mataji yake mjini Beijing mwezi ujao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Iddi Sessanga