1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bonn baada ya Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya

14 Septemba 2016

Uamuzi wa Waingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kupitia kura ya maoni ya Juni 23 bado unaendelea kuyatikisa maeneo mengine ya Ulaya, hata kwa mji mmoja mmoja kama ulivyo mji mkuu wa zamani wa Ujerumani, Bonn.

https://p.dw.com/p/1K0oK
Deutschland Bonn - "British shop" in Bonn
Ujumbe mzito mlangoni mwa dukaPicha: DW/P. Kwigize

Tukio hili lilitikisa dunia zikiwemo nchi zilizotawaliwa na Uingereza hasa Barani Afrika na Australia.

Tangu maamuzi hayo kufanywa na waingereza na kusababisha mshtuko kwa nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya, mazungumzo na maoni kuhusu tukio hilo yameendelea.

Kwa wakazi wa Ulaya wenyewe kila mmoja ana maoni yake, wapo wanaounga mkono na wapo wanaoona kuwa jambo hilo ni hatari kwa umoja huo kiuchumi na kidiplomasilia.

Deutschland Bonn - "British shop" in Bonn
Mwandishi wa habari wa DW Bw. Prosper Kwigize katika picha ya pamoja na muuzaji na msimamizi mkuu wa duka la kiingereza (England Shop) Bw. Beavan (kushoto) mwenye fulana yenye jina la duka.Picha: DW/P. Kwigize

Mji wa Bonn nchini Ujerumani ni moja ya maeneo muhimu katika Umoja wa Ulaya, hii ni kutokana na kwamba ulikuwa ni makao makuu ya serikali ya Ujerumani Magharibi wakati wa utawala wa Ujerumani mbili zilizotengwa na ukuta wa Berlin.

Katika mji huo adhimu kwa historia ya Umoja wa Ulaya, mkazi mmoja ameanzisha duka na kuliita "Duka la Kiingereza" na kuchapisha ujumbe mzito unaoshajihisha kuwepo kwa Ulaya moja.

Huyo si mwingine ni Bw. James Beavan; yeye anaamini kuwa maamuzi yaliyofanywa na Uingereza hayana maana kabisa hasa kwa vijana ambao matumaini yao makubwa ni kuona Ulaya moja iliyoungana na yenye nguvu kuliko wakati wowote.

Deutschland Bonn - "British shop" in Bonn
Duka kubwa la kiingereza katika mji wa Bonn lenye ujumbe wa UmojaPicha: DW/P. Kwigize

"Katika kila mji wa nchi yoyote ya Umoja wa ulaya wapo vijana kutoka Uingereza au Scotland, wanaishi vizuri lakini sasa wamejaa hofu baada ya maamuzi ya nchi yao, kwa wanaofanya biashara, wamekumbwa na mshtuko wakihofia kuwa huenda maazimio hayo yakawazuia kuishi katika nchi nyingine za Umoja huo wa Ulaya, "anasema Beavan

Ameeleza kuwa chanzo cha kuandika ujumbe katika mlango wa duka ni kuwatoa hofu wananchi, ambao huenda waliamini kuwa uamuzi wa kujiondoa kwa Uingiereza katika umoja wa Ulaya ndio mwisho wa mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara.

Asilimia 78 ya waingereza walijitokeza kupiga kura ya kusalia au kujiondoa na asilimia 52 walipiga kura ya kuachana na Umoja wa Ulaya wakati asilimia 48 wakipiga kura ya kuitaka Uingereza isalie katika Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Prosper Kwigize

Mhariri:Yusuf Saumu