1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

190710 BL-Porträt Dortmund

Aboubakary Jumaa Liongo20 Agosti 2010

Msimu mpya wa ligi ya kandanda ya daraja la kwanza ya Ujerumani, Bundesliga umeanza jana.Miongoni mwa timu zinazoshiriki ligi hiyo ni Borussia Dortmund.

https://p.dw.com/p/OshO
Wachezajai wa Dortmund wakishangilia ushindi katika moja ya mechi zaoPicha: AP

Ukianzia kusema, rangi nyeusi na njano au BVB basi yeyote aliyekuwa shabiki wa soka nchini Ujerumani anajua unamaanisha klabu gani.

Borussia Dortmund ilianzishwa mwaka 1909 kiasi ya miaka 101 iliyopita. Wakati huo ilikuwa ni jumuiya ya vijana wa kikatoliki waliyokuwa chini ya mpango maalum wa kucheza soka.

Kutokana na jumuiya hiyo ndipo ilipoanzishwa klabu ya Borussia 09 Dortmund.

Leo hii Borussia Dortmund inahesabiwa kuwa ni mojawapo ya vilabu vikubwa vya kandanda nchini Ujerumani, na inajivunia kuwepo katika jukwaa la kandanda barani Ulaya.

Imeshinda ubingwa wa Bundesliga mara sita, kombe la chama cha soka cha Ujerumani mara mbili, kombe la washindi barani Ulaya mwaka 1966 ambalo hivi sasa ni kombe la Ulaya.

Lakini mafanikio makubwa ni mwaka 1997 wakati ilipofanikiwa kutwaa ubingwa wa vilabu barani Ulaya kwa kuichapa Juventus Turin ya Italia mjini Turin mabao 3-1, huku chipukizi Lars Ricken akiwahukumu Wataliano kwa mkwaju maridadi aliyoufyatua kutoka umbali wa mita 30.

Ikiwa na furaha ya kushinda ubingwa huo wa Ulaya , Borussia Dortmund mwaka huo pia ikashinda ubingwa wa dunia.

Mwaka 2000 Borussia Dortmund iliingia katika soko la hisa na mpaka leo hii ndiyo klabu pekee ya Ujerumani iliyoko katika soko hilo. Miaka miwili baadaye mpaka sasa Dortmund walishinda ubingwa wa Ujerumani.

Baadaye hata hivyo ikabakia kuwa si timu ya ushindani. Madeni, kuuzwa kwa wachezaji wazuri, pamoja na uwanja wao vilitishia klabu hiyo kuwa muflisi.

Mwaka 2005 Borussia Dortmund ilijaribu kurejea katika hali yake ya kawaida, hata hivyo kwa washabiki hali ilikuwa ngumu kwao kushangilia.

Kocha wa timu hiyo Jürgen Kloop kwa miaka miwili alipoichukua timu hiyo, alikumbana na jukumu kubwa. Katika msimu uliyopita wa Bundesliga, Borussia Dortmund ilikamata nafasi ya tano na hivyo kupata nafasi ya kucheza katika mechi za kupata nafasi ya kuingia kwenye ligi ya mabingwa ya Ulaya. Na hapo juzi katika michuano ya Ulaya, Dortmund ilianza vyema kwa kuishindilia FK Qarabag ya Azerbaijan mabao 4-0, na kocha Kloop anasema

Flash-Galerie Fußball Bundesliga 2010/2011 Borussia Dortmund
Kikosi cha Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa

Baada ya kuwa miongoni mwa kilabu kubwa,lakini isiyokuwa na mustakbali,si rahisi-,ndiyo maana tunahitaji uvumilivu.Tunataka kushinda mechi zote kama ilivyokuwa zamani-Kwa sasa hilo haliwezekani na lazima mtu awe na subira´´

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Hans-Joachim Watzke amesema ni lazima Dortmund ijitegemee.

Ni lazima tuwaandae nyota wetu wenyewe, hatuwezi kununua wachezaji kama wengine wanavyofanya, kwani tunawajibika kushughulikia madeni yetu´´

Katika msimu huu mpya uliyoanza jana imefanikiwa kuwanasa wachezaji kadhaa, ambapo iliweza kuvunja kabati lake na kutoa kitita cha Euro millioni 4.5 kumnunua mchezajii wa timu ya taifa ya Poland mwenye umri wa miaka 22, Robert Lewandowski.

Wengine iliyowasajili msimu huu ni Kiungo mshambuliaji kutoka Japan Shinji Kagawa mwenye umri wa miaka 21, Mitchel Langerak mlinda mlango kutoka Australia na beki kutoka Poland, Lukasz Piszczek.

Dortmund inaanza safari yake ya kuwania taji la Bundesliga hii leo kwa kupambana na Bayer Levekusen ambayo imejiimarisha kwa kumsajili nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack, kutoka Chelsea ya Uingereza.

Mwandishi: Faupel, Sarah/Liongo, Aboubakary Jumaa

Mhariri:Josephat Charo