1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bozize ataka kuunda serikali na waasi

31 Desemba 2012

Wakati Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati akisema kuwa yuko tayari kugawana madaraka na viongozi wa kundi la waasi wa Seleka na kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa, waasi wamesema haja yao si madaraka.

https://p.dw.com/p/17BUv
Rais Francois Bozize.
Rais Francois Bozize.Picha: Reuters

Pamoja na ahadi ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, Rais Bozize pia amesema kuwa hatagombea tena muhula mwingine wa utawala katika uchaguzi wa mwaka 2016. Kauli hiyo ya Bozize imetolewa baada ya mazungumzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Thomas Boni Yayi.

Boni Yayi, ambaye ni Rais wa Benin, amesema kuwa Bozize yuko tayari kushiriki mazungumzo ya amani baina ya serikali yake na waasi ambayo yameandaliwa na Umoja wa Afrika mjini Libreville, Gabon ambayo yatakamilisha nia yake hiyo ya kuunda serikali ya pamoja.

Waasi wafikiria ahadi ya Bozize

Kwa upande wao waasi wa Seleka ambao kwa sasa wako umbali wa kilometa 75 nje ya mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, wamesema kuwa wanalifikiria tangazo hilo la Bozize. Msemaji wa muungano wa Seleka Eric Massi amekiamba kituo cha televisheni cha France 24 kuwa kwanza watakaa mezani kuangalia yaliyomo kwenye ahadi hiyo.

Rais Francois Bozize akizungumza mbele ya wafuasi wake.
Rais Francois Bozize akizungumza mbele ya wafuasi wake.Picha: AFP/Getty Images

Massi ameongeza kuwa wao haja yao ya msingi si madaraka bali ni kuwawezesha wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kupata maendeleo stahiki na kuweza kujitegemea kiuchumi.

Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari zinasema kuwa waasi huenda wakaingia mjini humo hii leo, ambako tayari amri ya kutotembea ovyo imetolewa.

Wasiwasi watanda Bangui

Maelfu ya wakaazi wa mji mkuu huo wameyakimbia makaazi yao wakihofia usalama wao. Waliosalia wamekusanya shehena za vyakula na maji majumbani mwao wakijiandaa endapo waasi wataingia mjini humo. Mitaa iko kimya kutokana na kutangazwa kwa hali ya hatari na matembezi ya usiku yamezuiwa.

Wafuasi wa Rais Bozize wakiandamana kutaka jumuiya ya kimataifa imsaidie kiongozi wao.
Wafuasi wa Rais Bozize wakiandamana kutaka jumuiya ya kimataifa imsaidie kiongozi wao.Picha: Reuters

Mkuu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka mjini Bangui, Sylvain Groulx, alikiambia kituo cha televisheni cha Aljazeera kuwa wasiwasi wao uko kwa watu waliokimbilia msituni baada ya kusikia milio ya risasi.

Harakati za wiki tatu za waasi hao kulekea mji mkuu wa Bangui zimezua taharuki miongoni mwa raia wa koloni hilo la zamani la Ufaransa. Nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa masikini zaidi duniani licha ya utajiri mkubwa wa madini ya Urani, almasi na dhahabu iliyonayo.

Hata hivyo bado haijafahamika kama fursa hiyo ya kuunda serikali ya pamoja iliyotolewa na Bozize itakuwa dawa sahihi ya mzozo huo ambao unatishia miaka kumi ya utawala wake. Waasi wa Seleka wanamtuhumu Rais Bozize kwa kukiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2007 ambapo wapiganaji waliokubali kuweka chini silaha zao walipaswa kulipwa.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail