1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi ziarani China

MjahidA31 Oktoba 2012

Mjumbe maalum wa Kimataifa juu ya Syria, Lakhdar Brahimi amesema hii leo, kwamba anatumai China itachangia kwa kiasi kikubwa katika kupatikana amani nchini Syria.

https://p.dw.com/p/16Zw0
Brahimi na Yang kwenye mazungumzo katika wizara ya mambo ya nje China
Brahimi na Yang kwenye mazungumzo katika wizara ya mambo ya nje ChinaPicha: picture-alliance/dpa

Brahimi aliyasema hayo alipokutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa China, kwa mazungumzo katika ziara yake ya siku mbili nchini humo.

Akisalimiana na waziri yang Jiechi mbele ya waandishi habari, Brahimi alisema anatumai China itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukomesha mapigano Syria, ingawa hakueleza zaidi juu ya tamko lake hilo. China kwa sasa ina wasiwasi juu ya kuingiliwa kwa mambo ya ndani ya nchi nyingine.

China na Urusi zimekuwa zikitumia kura ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kupinga maazimio ya kumshinikiza Rais Bashar Al Assad kukomesha mapigano Syria. Yang alimshukuru Brahimi kwa kazi yake huku akisema anatumai pia mazungumzo yao ambayo ni ya tatu ndani ya miezi miwili, yatafanikiwa kuchangia katika kuutatua mgogoro wa Syria.

Waziri wa mambo ya nje China, Yang Jiechi
Waziri wa mambo ya nje China, Yang JiechiPicha: AP

Hata hivyo wizara ya mambo ya nje nchini China haikutoa maelezo zaidi juu ya mazungumzo ya Lakhdar na Yang lakini ikasema kuwa china itajaribu kupitisha azimio la kisiasa Syria. Msemaji wa wizara hiyo Hong Lei amesema china imekuwa ikijaribu kupitisha azimio la kisiasa katika mzozo wa syria na itaendelea kufanya hivyo huku ikiendelea pia kufanya kazi na jamii ya Kimataifa.

Wachambuzi wanasema kusita kwa China kuunga mkono maazimio yoyote juu ya Syria kunatokana na namna mataifa ya magharibi yalivyoiingilia kijeshi Libya hatua iliouangusha utawala wa Muammar Gaddafi. China ilipinga Libya kuingiliwa kijeshi lakini haikutumia kura yake ya turufu Machi 2011 katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, hatua ilioidhinisha kitendo hicho. China inasema kuwa jamii ya kimataifa ilivuka mipaka wakati wa ghasia za Libya.

Brahimi aliyechukua wadhifa huo baada ya kujiondoa kwa Koffi Annan kwa kile alichokiita kutoungwa mkono na mataifa ya Magharibi, anatarajiwa kutoa mapendekezo mapya ya namna ya kusuluhisha mzozo wa Syria katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi ujao.

Mapigano zaidi Syria

Huku hayo yakiarifiwa wanaharakati nchini Syria wamesema hii leo vikosi vya serikali vimepambana na waasi walioanzisha mashambulizi dhidi ya vituo vya ukaguzi vya kijeshi katika mkoa wa kaskazini wa Idlib. Katika shambulizi hilo wanajeshi wanne waliuwawa huku wengine kumi wakijeruhiwa.

Ndege ya kivita Syria
Ndege ya kivita SyriaPicha: AFP/GettyImages/Tauseef Mustafa

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake mjini London Rami Abdel Rahman, amesema helikpopta moja ya kijeshi ilidunguliwa na waasi.

Pia kumeripotiwa mashambulizi ya angani mjini Maaret al-Numan, mji unaoshikiliwa na waasi. Rami Abdul-Rahman amesema watu 185 waliuwawa katika mashambulizi ya jana.

Tangu kuanza kwa mapigano nchini Syria miezi 20 iliopita watu zaidi ya 35,000 wameuwawa huku wengine wengi wakipoteza makaazi yao.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri Yusuf Saumu