1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil kuumana na Uhispania katika fainali

28 Juni 2013

Dimba la Kombe la Mabara limefikia fainali iliyosubiriwa na wengi. Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia dhidi ya mabingwa mara tano. Mabingwa mara mbili wa Ulaya dhidi ya wenyeji wa dimba hilo la Confederations Cup

https://p.dw.com/p/18yDb
Spain's Sergio Ramos (R) gestures as he celebrates after Jesus Navas scored the winning penalty goal against Italy during the penalty shootout of their Confederations Cup semi-final soccer match at the Estadio Castelao in Fortaleza June 27, 2013. REUTERS/Jorge Silva (BRAZIL - Tags: SPORT SOCCER) / Eingestellt von wa
Confederations Cup / Spanien - Italien / SiegtrefferPicha: Reuters

Magwiji wa kupiga pasi fupi na za uhakika, dhidi ya nyota mpya wa Brazil Neymar. Uhispania walifuzu katika fainali baada ya mchuano mkali wa kuchosha ambapo walishinda kwa mikwaju ya panalti walipoifunga Italia mabao saba kwa sita na sasa watapambana na Brazil katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro kesho Jumapili, na kuteremsha pazia la kinyang'anyiro hicho cha kupasha misuli moto kabla ya tamasha lenyewe la kombe la dunia hapo mwakani nchini humo.

Nahodha wa Uhispania Iker Casillas anasema anafikiri kuwa kila mmoja alikuwa akisubiri fainali kati ya Uhispania na Brazil na kwa mtazamo wake, timu mbili ambazo zinastahili kucheza katika fainali ndizo zilizofuzu. Lakini wakati dimba hilo likifikia ukingoni, kumekuwa pia na maandamano makubwa katika miji mikubwa ya kulalamikia huduma duni za umma pamoja na ufisadi serikali.

Wenyeji Brazil walifuzu katika fainali kwa kuwabwaga mahasimu wao Uruguay mabao 2 - 1
Wenyeji Brazil walifuzu katika fainali kwa kuwabwaga mahasimu wao Uruguay mabao 2 - 1Picha: picture-alliance/dpa

Kabla ya mechi ya nusu fainali kati ya Uhispania na Italia, takribani watu 5,000 walipambana na polisi karibu kilomita mbili kutoka uwanja huo wa michezo. Maandamano zaidi ya kuipinga serikali yanatarajiwa kufanyika kesho Jumapili wakati wa fainali ya dimba hilo.

Jumapili itakuwa fainali ya nne kubwa kwa Uhispania kuwahi kucheza katika miaka mitano, baada ya kushinda kombe la mataifa ya Ulaya mwaka wa 2008 na 20012 pamoja na kombe la dunia mwaka wa 2010. Katika mchuwano wa kumpata mshindi wa tatu, Uruguay itamenyana na Italia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters

Mhariri: Yusuf Saumu