1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil na Afrika

5 Julai 2007

Ushirikiano kati ya Brazil na Afrika unazidi kuimarika b aada ya Brazil kuanza kuweka umuhimu zaidi kati yake na nchi za kusini za sayari hii.Rais Lula amezuru nchi 17 za Afrika na viongozi wengi wa Afrika wamewasili Brazil.

https://p.dw.com/p/CHBa

Jana ulifanyika mkutano wa kilele kati ya Brazil na Umoja wa ulaya mjini Lisbon,Ureno.Uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini ni mojawapo ya sera za usoni kabisa za serikali ya ureno, mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya.

Lakini mbali na usuhuba na Ulaya na Marekani,Brazil imekuwa ikiimarisha hivi karibuni mafungamano yake na bara la Afrika.Wakaazi wengi wa mkoa wa Bahia,Brazil wana asili ya Afrika.

Yule anaeuangalia utajiri wa Afrika kwa jicho la mali zake asili tu,huyo amepotea njia.Bara la Afrika lina mengi ya kuutajirisha ulimwengu.Mfano katika nishati ya kimazingira.

Fernando Jacques wa wizara ya nje ya Brazil asema:

“Nchi za kiafrika zina mali nyingi asili ya kutengezea nishati isiochafua mazingira kwavile ina mazao mengi yanayofaa kutengezewa nishati hiyo.Katika sekta hii tunaweza kuwapa waafrika utaalamu wetu.”

Tayari katika miaka ya 1980 mafuta ya Ethanol yakitengezwa kutoka miwa ili kuendeshea sehemu kubwa ya magari nchini Brazil.Taftishi na maendeleo ya nishati ya aina hii ya kimazingira zinaendelea kupewa shime nchini Brazil.

Na sio tu kutokana na miwa bali pia mhogo na njugu za Rizi hutengezwa nishati ya kuendeshea magari.Wakati Botswana huko kusini mwa Afrika kwa mfano inavuna mbarika kwa wingi mno,Tanzania inavuna mihogo mingi.Wengine waona katika miwa kuna matumaini makubwa ya kutengeza nchini mafuta ya Ethnol.

Fernando Jacques anaongeza:

“Hii tu haizivutii nchi ambazo hazitoi mafuta ya petroli bali mazao hayo yanapunguza kutegemea petroli.Na hii, yaweza kupelekea kupunguza tangu matumizi hata gharama za kuagiza mafuta kutoka nje kwa nchi hizo.”

Lakini hata kwa nchi zinazotoa mafuta zaweza kuwa na hamu ya kujipatia nishati ya mafuta yanayotokana na mimea kwavile nishati ya aina hiyo yaziwezesha nchi kama hizo kujiandaa kwa siku moja ambapo akiba zao za mafuta zimemalizika.

Lakini ushirikiano wa pande hizi mbili za kusini-Brazil na Afrika haumalizikii katika sekta ya nishati.Brazil inatoa nafasi nyingi za masomo ya vyuo vikuu kwa nchi nyingi za Afrika.

Ingawa ushirikiano katika sekta ya elimu umeegemea zaidi koloni za zamani za ureno kama zinazozungumza kireno kama Msumbiji,Angola au visiwa vya Cape Verd,mpango wa elimu wa Brazil milango yake ni wazi hata kwa nchi nyengine shirika.Kwa njia hii, mnamo miaka 5 iliopita idadi ya wanafunzi wa kiafrika katika vyuo vikuu vya Brazil imefikia 240.

Hata katika sekta ya afya Brazil imewasili Afrika:

Mfano nchini Nigeria,ambako ni asili ya wakaazi wengi wa mkoa wa Bahia wa Brazil wa asili ya Yoruba na hata Msumbiji Brazil inachangia mno katika vita vya kupambana na kifua kikuu na UKIMWI.

Katika sekta ya kiuchumi kampuni la mafuta la Brazil “Petrobras” linashirikiana mno katika uchimbaji mafuta nchini Nigeria,Angola,Tanzania,Equitorial Guinea na Libya.

Pekee tangu 2003,Brazil imefunga mikataba ya pande mbili zaidi ya 100 na nchi za kiafrika.

Katika kipindi chake tangu kushika wadhifa wa urais,rais Lula amezuru jumla ya mataifa 17 ya kiafrika.Pia amewapokea Brazil viongozi kadhaa wa Afrika.

Kwahivyo, biashara kati ya Brazil na Afrika baina ya 2002 na 2006 imeongezeka mara 4.Kutoka dala bilioni 5 imepanda hadi bilioni 15.

Jicho la Brazil halielekezwi tena kama hzamani upande mmoja tu wa kaskazini.Leo hii siasa yake ya nje inatupa macho zaidi na zaidi kusini.Shabaha ni jeografia na ramani mpya ya usuhuba wa kibiashara.