1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil, Uholanzi, Mexico na Chile zafuzu 16 bora

24 Juni 2014

Wenyeji Brazil wameweka miadi ya kukutana na Chile katika hatua ya 16 bora baada ya kuigagadua Cameroon kwa magoli 4-1. Mexico itamenyana na Uholanzi baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Croatia.

https://p.dw.com/p/1COhK
Mchezaji wa Cameroon Eyong Enoch akimkabili Neymar wa Brazil
Mchezaji wa Cameroon Eyong Enoch akimkabili Neymar wa BrazilPicha: picture-alliance/dpa

Mchezaji Neymar ndiye alifungua karama ya magoli ya Brazil katika dakika ya 17, akiweka kimyani goli lake la tatu la mashindano haya, na kufikisha jumla ya magoli katika mashindano ya Brazil 2014 hadi 100 wakati wa mechi ya 100 ya kombe la dunia ya wenyeji hao.

Mchezaji Joel Matip aliipatia Cameroon goli la kusawazisha na la kwanza katika mashindano ya mwaka, huu chini ya dakika 10 baadaye, akifunga kwa mpira wa Allan Nyom, ambaye alitumia vyema makosa ya mlinzi Dani Alves kushoto mwa boxi la Brazil.

Neymar alifunga bao lake la pili la mchezo huo na la nne katika mechi tatu, na kuipa Brazil uongozi wa mabao 2-1 dakika kumi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Fred aliifungia Brazil goli la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili, na mchezaji wa akiba Fernandinho alihitimisha na la nne dakika tano kabla ya firimbi ya mwisho.

Ivica Olic wa Croatia dhidi ya Rafael Marques wa Mexico
Ivica Olic wa Croatia dhidi ya Rafael Marques wa MexicoPicha: Reuters

Ushindi huo ulikuwa ni ahueni kwa wenyeji hao baada ya mwanzo wa mashindano usiyoridhisha kutilia mashaka hadhi yao kama moja ya timu zinazopewa nafasi ya kubeba kombe la mwaka huu. Ushindi huo umewaacha katika uongozi wa kundi A, mbele ya Mexico ambayo iliwabana mbavu kwa sare tasa.

Mexico yaigeuza Croatia "ngazi"

Mexico ilijihakikishia nafasi katika raundi ya pili ya mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya sita mfululizo kwa kushindilia Croatia magoli 3-1. Rafael Marquez, Andre Guadado na Javier "Chicharito" Hernandez wote walifunga katika muda wa dakika 10 na kuiangamiza timu yenye vipaji ya Croatia kwenye hatua ya makundi.

Wacroatia walitakiwa kushinda ili kuweza kusonga mbele, na walimiliki mpira kwa sehemu kubwa, lakini walipata tabu kuliona lango la Guillermo Ochoa, ambaye alizuwia juhudi zao zote hadi goli la kufutia machozi la dakika ya 87 lililofungwa na Ivan Perisic.

Mexico waliingia katika mchezo wa jana wakihitaji tu sare na walionekana kuwa wa hatari katika mashambulizi, lakini Croatia iliwamudu hadi mpasuko wa magoli matatu. Alikuwa Marques alieshambulia kwanza, akimpiga chenga mlinzi wa Croatia Vedran Corluka na kuweka kimyani mpira wa kona iliyopigwa na Hector Herrera katika dakika ya 72.

Dakika tatu baadaye, Guardado alizitikisa nyavu kwa mkwaju mzito kufuatia krosi kutoka kwa Oribe Peralta. Na baadaye katika ya 82, mchezaji maarufu wa Manchester United Hernandez, ambaye amekuwa mchezaji wa akiba wa kipindi cha pili katika mechi zote tatu za Mexico, alifunga kwa kichwa kufuatia kona ya Herrera.

Mexico sasa watacheza dhidi ya Uholanzi, ambao walimalizia usukani mwa kundi B, baada ya kuishinda Chile kwa magoli 2-0 katika mchezo uliyotangulia.

Arjen Robben wa Uholanzi akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Chile.
Arjen Robben wa Uholanzi akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Chile.Picha: Reuters

Roy Hodgson kuchezesha chipukizi dhidi ya Costa Rica

Leo jioni, England itatumia wachezaji chipukizi katika mechi yake dhidi ya Costa Rica mjini Belo Horizonte, katika mechi ambamo taifa hilo la America ya kati linalenga kukaa usukani mwa kundi, huku England ikipigana kulinda heshima yake.

Costa Rica wamekuwa moja ya maajabu makubwa ya michuano ya kombe la dunia mwaka huu wa 2014, kwa kufuzu raundi ya 16 bora na ushindi dhidi ya mabingwa wa zamani Uruguay na Italia. Ikiwa watapata alama angalau moja katika mchezo wao dhidi ya England wataongoza kundi lao.

Kocha wa England Roy Hodgon alisema ingawa timu tayari imekwishaondolewa kutoka mashindano ya kombe la dunia, atachezesha kikosi mbadala ili kuwapa wachezaji wake wote ladha ya mchezo wa kombe la dunia.

Katika mchezo mwingine wa kundi D Italia itachuana na Uruguay. Japan itacheza dhidi ya Colombia na Ugiriki itamenyana na Cote d'voire katika michezo ya kundi C.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo