1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brazil yasisitiza itakuwa tayari kwa Kombe la Dunia

30 Novemba 2013

Mhandisi wa masuala ya usalama katika uwanja wa Sao Paolo ambako kreni kubwa iliporomoka inadaiwa alimwonya msimamizi wake kuhusu uwezekano wa kuwepo matatizo katika operesheni hiyo, na kisha ilani yake ikapuuzwa.

https://p.dw.com/p/1AR4o
Picha: Miguel Schincariol/AFP/Getty Images

Watu wawili walipoteza maisha yao kutokana na ajali hiyo. Tukio hilo limezusha wasiwasi kuhusiana na uwezo wa Brazil kuandaa dimba hilo la mwaka ujao, pamoja na michezo ya Olimpiki mwaka wa 2016, ijapokuwa maafisa wanasisitiza kuwa nchi hiyo itakuwa tayari kwa matamasha hayo mawili.

Uwanja wa Sao Paolo Arena Corinthians ulitarajiwa kukamilishwa ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Desemba, na wafanyakazi wamedokeza kuwa kasi hiyo ilikuwa suala la kipau mbele katika ujenzi wa uwanaj huo, huku wengi wakifanya kazi kwa zamu za saa 12 na kunyimwa mapumziko.

Shirikisho la Soka duniani FIFA limesema linasubiri kufahamiswha kuhusu kiwango cha uharibifu kutokana na ajali hiyo ya Jumatano wiki hii. Maafisa wa FIFA pamoja na viongozi wengine wa kabumbu ulimwenguni wanatarajiwa kuwasili nchini Brazil wiki ijayo kwa ajili ya droo inayosubiriwa kwa hamu na ghamu ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia mjini Costa do Sauipe.

Viongozi wa FIFA wanasisitiza kuwa hakuna mpango mabadala kwa dimba hilo la mwaka ujao, na hasa kwa sababu karibu tikiti milioni moja za mechi hizo tayari zimeuzwa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Mohammed Dahman