1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit kughubika mkutano wa EU na nchi za Ulaya Mashariki

Daniel Gakuba
24 Novemba 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanashiriki katika mkutano wa kilele ambao agenda yake kuu ni ushirikiano na nchi sita za Mashariki mwa Ulaya. Hata hivyo vikao vya pembezoni kuhusu mchakato wa Brexit kuipiku agenda hiyo.

https://p.dw.com/p/2oBBD
Belgien EU-Gipfel Theresa May und Donald Tusk
Mazungumzo kuhusu Brexit yanaweza kuipiku agenda ya mkutano ambayo ni ushirikiano na nchi za Ulaya MasharikiPicha: Reuters/G. Vanden Wijngaert

Huu ni mkutano wa kilele wa tano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi hizo za Mashariki mwa Ulaya, ambazo ni Armenia, Azerbaijan, Belarus, Georgia, Moldova na Ukraine, ambazo tangu mwaka 2009, juhudi zimekuwa zikifanyika kuzisogeza karibu na Ulaya kisiasa na kiuchumi. Umoja wa Ulaya unachukua tahadhari katika juhudi za kuimarisha uhusiano huo unaojulikana kama 'Ushirikiano wa Mashariki' ili usijiingize katika mvutano na Urusi ambayo inaweza kuzichukulia hatua hizo kama uingiliaji katika eneo lake la ushawishi.

Mkutano wa leo unafanyika yakiwepo mafanikio ya hivi karibuni katika kuwaondolea visa raia wa Ukraine na Georgia wanaotaka kuzuru nchi za Umoja wa Ulaya. Mazungumzo yatahusu namna ya kuboresha hali ya ushirikiano wa kijamii, kiuchumi na kiutawala katika nchi hizo sita za Mashariki zinazoshiriki.

Lukashenko aususia mkutano huo

Nchi tano kati ya hizo; Ukraine, Moldova, Georgia, Azerbaijan na Armenia zinawakilishwa na marais, lakini Belarus inasimamiwa na waziri wake wa mambo ya nchi za nje, licha ya kwamba mwaliko ulitumwa moja kwa moja kwa rais wa nchi hiyo, Alexander Lukashenko, ambye ni rafiki mkubwa wa Urusi. Huu ulikuwa mwaliko wa kwanza kwa rais huyo, ambaye wakati wa mikutano iliyotangulia alikuwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Deutschland Angela Merkel nach dem Ende der Sondierungsgespräche
Bi Angela Merkel mara hii anahudhuria kama Kaimu Kansela wa UjerumaniPicha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

Macho lakini yataelekezwa zaidi katika mazungumzo ya pembezoni baina ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, kuhusu hatima ya mchakato wa Uingereza kujitoa ndani ya Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit. Alipowasili Brussels, Theresa May amesema mafaniko katika mazungumzo ya Brexit ni kwa maslahi ya pande zote mbili.

''Nitakutana na Rais Donald Tusk leo, kuzungumzia mafanikio yaliyofikiwa, nikitazamia kupatikana mustakabali mwema wa ushirkiano ambao nautaka kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza.'' amesema Bi May na kuongeza, ''Ninachojua dhahiri ni kwamba tunalazimika kupiga hatua pamoja. Ni kwa maslahi ya pande zote mbili kusonga mbele.''

EU yatazamia pendekezo jipya la Uingereza

Baada ya miezi kadhaa ya mkwamo katika mazungumzo yanayohusiana na mchakato huo, viongozi wa Ulaya wanatumai kwamba hatimaye Bi May ataleta pendekezo jipya kuhusu kiwango cha fedha ambacho nchi yake iko tayari kukilipa, baada ya mawaziri muhimu wa Uingereza kukubaliana wiki hii kuongeza kiwango hicho hadi euro bilioni 40.

Belgien EU-Gipfel Jean-Claude Juncker
Rais wa Baraza la Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Reuters/D. Pignatelli

Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker amesema inabidi ifahamike wazi kwamba mazungumzo haya hayahusu uwanachama wa nchi hizo sita za Mashariki mwa Ulaya, bali ushirikiano katika nyanja mbali mbali, ambao amesema unaendelea vyema, japo haridhiki na kila kitu.

Bi Angela Merkel ambaye hivi sasa ni kaimu Kansela wa Ujerumani atahudhuria mkutano huo wa kilele, baada ya kutoshiriki katika kikao cha wiki iliyopita nchini Sweden, kwa sababu alikuwa akijikita katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto wa vyama ambayo sasa yamevunjika.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe, dw

Mhariri: Mohammed Khelef