1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Brexit" Uingereza haina mpango maalum

Zainab Aziz
15 Novemba 2016

Taarifa iliyovuja yaonyesha Uingereza haina mpango maalum wa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Mgawanyiko ndani ya baraza la mawaziri huenda ukachelewesha kwa miezi sita, mchakato wa kuanza mazungumzo ya kujitoa. 

https://p.dw.com/p/2Sk4s
Großbritannien Europaflagge vor dem Big Ben in London
Picha: picture alliance/empics/D. Leal-Olivas

Taarifa hiyo ambayo inaaminiwa kuwa imetayarishwa na mshauri maalum kwa ajili ya kitengo cha serikali kinachomsaidia waziri mkuu Theresa May na baraza lake la mawaziri inaashiria kuwepo kwa kuchanganyikiwa maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Uingereza katika swala la nchi hiyo la kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.  Bibi May anajaribu kushughulikia mwenyewe maswala muhimu kuhusu mpango huo, huku mawaziri wake wakikumbwa na mgawanyiko. Taarifa hiyo inatilia shaka endapo njia anazozitumia waziri mkuu huyo wa Uingereza za kufikia maamuzi zitafaulu.

Msemaji wa Ofisi ya waziri Mkuu hata hivyo amekanusha kuhusika ofisi hiyo au serikali kwa jumla na taarifa hiyo iliyovuja ingawa hakukanusha pia iwapo ni ya kweli au la.  msemaji huyo aliendelea tu kusema kuwa waziri mkuu Theresa May anatilia maanani kufanikiwa kwa mpango wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu Brexit.  Taarifa hiyo iliyovuja inaipa sura ya kushindwa serikali ya Uingereza  katika mchakato huo, na  pia inaonyesha wasiwasi uliopo kwa siku za usoni wakati ambapo bibi May anajaribu kuitoa Uingereza kutoka kwenye muungano mkubwa wa kibiashara barani Ulaya.

Indien Großbritannien Besuch von Theresa May bei Narendra Modi
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/dpa/H. Tyagi

Baraza la mawaziri chini ya uongozi wake bibi Theresa May limegawanyika baina ya mawaziri waliounga mkono kujiondoa na wale waliotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya. Waziri wa mambo ya nje Boris Johnson, waziri wa uchumi Liam Fox na waziri wa Brexit David Davis walikuwa tangu mwanzo katika kambi ya kujiondoa huku wanaotaka kubakia wakiwa ni pamoja na waziri wa fedha Philip Hammond na waziri wa nishati na viwanda Greg Clark.

Taaifa hiyo inamtaja bibi May kuwa anaelekeza bidii yake katika kukiweka chama chake pamoja kuliko kuyapa kipaumbele maswala ya biashara na uchumi. Idara za serikali zinaendelea kuifanyia kazi zaidi ya mipango 500 inayohusiana na Brexit, takriban wafanyakazi 30,000 zaidi watahitajika ili kulifanikisha zoezi hilo.

May ameahidi kwamba mwishoni mwa mwezi Machi mwakani atakitumia kifungu cha 50 cha mkataba wa Lisbon ambacho kitaanzisha rasmi mazungumzo yatakayo dumu kwa miaka miwili mjini Brussels kuhusu namna Uingereza itakavyojiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Lakini iwapo mahakama kuu ya nchi hiyo itaamua kuilazimisha serikali iwape wabunge nafasi ya kuchangia mada ya Brexit basi baadhi ya mawaziri watafurahia kuona misimamo mikali ya kujiondoa huko ikipunguziwa umuhimu. Bibi May mpaka sasa hajaeleza kuhusu mipango ya Uingereza kuhusu uhusiano wake wa baadae na nchi zingine wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi Zainab Aziz/RTRE

Mhariri:Gakuba Daniel