1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brown achukua hatamu za kuiongoza Uingereza

Mohammed AbdulRahman27 Juni 2007

Malkia Elizabeth wa Uingereza amemuomba Brown mwenye umri wa miaka 56 na aliyekaua waziri wa fedha ,aunde serikali, baada ya Tony Blair kuwasilisha hati ya kujiuzulu, baada ya kuwa madarakani kwa muda wa miaka 10.

https://p.dw.com/p/CB3G
Waziri mkuu mpya mteule wa Uingereza Gordon Brown na mkewe kwenye makaazi yake mpya nambari 10 mtaa wa Downing mjini London.
Waziri mkuu mpya mteule wa Uingereza Gordon Brown na mkewe kwenye makaazi yake mpya nambari 10 mtaa wa Downing mjini London.Picha: AP

Gordon Brown sasa ana´vaa kofia mbili, baada ya kuchaguliwa wiki iliopita kukiongoza pia chama tawala cha Leba.Hapo kabla leo, Tony Blair aliondoka bungeni kwa mara ya mwisho na kuelekea kasri la Malkia Buckingham Palace kuwasilisha barua ya kujiuzulu. Wabunge walisimama kumpa heshima wakimshangiria katika hali ilionekana wazi kuwa ya shauku kubwa. Hayo yalitanguliwa na kikao cha masuali na majibu ambapo Blair alijibu juu ya Irak, Afghanistan na mashariki ya kati, lakini hakuomba radhi kwa msimamo wake wa kuiunga mkono Marekani katika hatua yake ya kijeshi nchini Irak.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani David Cameron alimpongeza binafsi Blair na kumtakia kila la heri pamoja na fanilia yake. Akijibu Blair naye alisema anamshukuru, lakini akaongeza kwa mzaha “ Wakati siwezi kukutakia mafanikio katika uwanja wa kisiasa, nakutakia kila la mafanikio katika maisha yako ya kibinafsi.”, huku baadhi ya wabunge wakiangua kicheko.Blair aliaga rasmi kwa kupiga picha akiwa na familia yake, mkewe na watoto wao wanne wavulana watatu na msichana mmoja, nje ya makaazi ya Waziri mkuu.

Kwa upande mwengine Gordon Brown alielekea kasri la Malkia ambaye alimuomba aunde serikali kama Waziri mkuu mpya, Akiingia katika makao makuu na makaazi ya Waziri mkuu nambari 10 mtaa wa Downing. Bw Brown alitoa taarifa yake kawa vyombo vaya habari nje ya makao hayo makuu akisema ameombwa na Malika aunde serikali na ana heshima kubwa kupewa wadhifa huo wa kuitumikia Uingereza .

Alisema ataunda serikali itakayokua na sifa akiwa na yakini hakuna lisiloweza kukabiliwa, kwa jitihada na utayarifu wa wananchi wa Uingereza . Awali aliwaaga watumishi wa Wizara yake ya fedha, ambapo aliiongoza tangu chama cha Leba kilipoingia madarakani 1997.

Baada ya miaka 10 ya kuwa madarakani kama Waziri mkuu, enzi ya Blair imemalizika na kuanza enzi mpya ya Gordon Brown.