1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Kansela Merkel ajaribu kupata maafikiano katika Umoja wa Ulaya

22 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBpP

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya katika mji mkuu wa Ubeligiji,Brussels umefikia hatua muhimu. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,alieshika wadhifa wa urais unaozunguka kila miezi sita katika Umoja wa Ulaya,anauongoza mkutano huo, akijaribu kupata makubaliano ya mkataba mpya.Kwa maoni yake,mkataba huo utarahisisha utaratibu wa kupitisha maamuzi katika Umoja wa Ulaya unaopanuka.Mkataba mpya unakabiliwa na upinzani mkali kutoka Uingereza,inayotaka kuhakikishiwa kuwa mkataba huo hautoingilia mamlaka ya kitaifa. Kwa upande mwingine,Poland inataka kuwa na usemi mkubwa zaidi katika mfumo wa kupiga kura uliopendekezwa.Kansela Merkel alikuwa na mazungumzo mbali mbali na viongozi hao wawili katika jitahada ya kuondosha wasiwasi wao. Makubaliano ya mkataba huo mpya,hayatazamiwi kupatikana,kabla ya usiku wa leo.Mkataba huo, utachukua nafasi ya katiba iliyokataliwa na wapiga kura nchini Uholanzi na Ufaransa,katika kura ya maoni iliyopigwa miaka miwili iliyopita.