1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Kosovo yatakiwa isitangaze uhuru kutoka kwa Serbia

20 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CP25

Mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels, Ubelgiji, wamewatolea mwito Walbania wa Kosovo wasitangaze uhuru kutoka kwa Serbia.

Akizungumza kandoni mwa mkutano huo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeir, amesema hatua hiyo itasababisha matatizo makubwa na kwamba suluhisho litakalofikiwa litafaa kwa pande zote husika.

´Tangazo la uhuru kutoka upande mmoja, litasababisha hatimaye kuwepo na watu wengi na pande nyingi zilizoshindwa kwa kuwa hivi sasa wazo hilo halileti maana ya kutosha.´

Kiongozi muasi wa zamani wa Albania, Hashim Thaci, ambaye chama chake kilishinda uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, ametishia kutangaza uhuru wa Kosovo ikiwa makubaliano kuhusu hatima ya jimbo hilo hayatafikiwa kufikia tarehe 10 mwezi ujao.