1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Marekani yataka NATO isaidie zaidi Afghanistan.

27 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCXY
Marekani imesema inapanga kuongeza msaada wake kwa Afghanistan kwa dola zaidi ya bilioni kumi kwa muda wa miaka miwili ijayo na wakati huo huo ikayataka mataifa ya muungano wa NATO kuendelea kukabiliana vilivyo na wanamgambo wa Taliban nchini humo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Bibi Condoleezza Rice alitangaza hayo mjini Brussels, Ubelgiji, kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa ya NATO.

Bibi Condoleezza Rice amekiambia kituo kimoja cha televisheni cha Ujerumani kwamba ni wazo zuri sana iwapo Ujerumani itakubali ombi la NATO la kupeleka ndege zake sita za kijeshi kusini mwa Afghanistan.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinemeier mapema aliwaambia waandishi wa habari kwamba harakati za kijeshi pekee haziwezi kuisaidia Afghanistan kuondokana na hali ngumu iliyopo sasa.

Duru zinasema wasimamizi wa kijeshi nchini humo wanapanga kutekeleza harakati kubwa ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Taliban.

Mwaka uliopita ghasia ziliongezeka nchini humo na kusababisha vifo vya watu alfu nne wakiwemo askari mia moja na sabini wa kigeni.