1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brussels: Matumaini ni 'suali la maisha'

26 Machi 2016

Zaidi ya watu 30 inaaminiwa walikufa katika mashambulizi ya Brussels wiki hii. Lakini mwandishi wa DW Kathleen Schuster anasema si kila mtu aliyekata tamaa kwamba jamaa wake asiyejulikana aliko, atarejea.

https://p.dw.com/p/1IK68
Belgien Brüssel Laurent DuHaut an Haltestelle Maalbeek
Laurent Duhaut katika kituo cha treni cha MaalbeekPicha: DW/K. Schuster

Wahanga wengi wa mashambulizi ya Brussels hawajathibitishwa wamekufa, hata wale ambao vyombo vya habari vimewaorodhesha katika orodha ya watu waliokufa. Hili ndilo jambo Laurent Duhaut aliloligundua alipoona picha ya rafiki yake wa karibu ikioneshwa katika televisheni kufuatia mashambulizi ya siku ya Jumanne asubuhi.

Oliver Delespesse ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza ambaye Duhaut alikutana naye siku ya kwanza katika chuo kikuu mwishoni mwa miaka ya 1990. Baada ya kuwa marafiki wakubwa, waliendelea kuwa na mahusiano ya karibu kwa miaka 20. Kwa Duhaut, Delespesse alikuwa sehemu ya kile kinachoufanya mji wa Brussels kuwa nyumbani.

"Tafrani ya siku ya Jumanne iliwaacha wengi bila taarifa kwa saa kadhaa. Saa zilipoendelea kupita, Duhaut na jamaa wa familia ya Delespesse waliingiwa na wasiwasi wakati waliposhindwa kuwasiliana naye." Muajiri wake, kampuni ya Wallonia-Brussels Federation, imesema aliuliwa wakati wa safari yake ya kawaida ya asubuhi. Hata hivyo, kwa mujibu wa Duhaunt, wachunguzi wamefaulu kuthibitisha tiketi yake ya treni inayosafiri katika njia ya chini ya ardhi ilipigwa picha katika mashine ya kuhakiki tiketi muda mfupi kabla bomu kulipuka katika kituo cha Maelbeek.

'Suali la maisha'

Maji ya mvua yanatiririka katika madirisha ya mgahawa ambamo Duhaut na Delespesse mara kwa mara walikuwa wakikutana kwa chakula au kinywaji. Ni siku ya Ijumaa Kuu, siku ya huzuni katika mataifa ya kikristo, na hususan leo katika mji wa Brussels, ni siku inayoshahibiana na huzuni iliyotanda katika mji unaojizatiti kulikabili janga lilitokea.

Baada ya karibu saa nzima ya kujadiliana na rafikii, picha za mtu huyo mwenye umri wa miaka 45 anayemueleza kama mtu aliyekuwa tayari kuzungumza na kushirikiana na watu wengine kutumia ucheshi yanasababisha machozi kutiririka katika macho ya Duhaut kwa mara ya kwanza.

Belgien Brüssel Laurent DuHaut
Duhaut alituma picha ya rafiki yake asiyejulikana aliko mtandaoni na akaiona ikioneshwa katika vyombo vya habari kama mmoja wa waathirika wa mashambuliziPicha: DW/K. Schuster

"Kwa sisi, bado angali hai mpaka tuone cheti rasmi cha kifo chake. Tutaendelea kuamini hivyo na kuendelea kumtumia nguvu chanya," anasema, akiongeza kwamba ni "suali la maisha."

Watu wapatao 300 walijeruhiwa katika mashambulizi ya uwanja wa ndege wa Brussels na kituo cha treni cha Maelbeek. Wengi pia walipoteza fahamu kabisa kufuatia uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo, anasema Duhaut. Uwezekano mwingine ni kwamba mwandani wake wa karibu amepoteza fahamu au ameumia mno kiasi cha kutoweza kutambulika.

Madaktari wakabiliwa na changamoto kubwa

Kilomita 30 mashariki mwa Brussels, madaktari wa upasuaji katika hospitali ya chuo kikuu cha Leuven - kituo kimojawapo kikubwa wanakofikia wahanga wa shambulizi la uwanja wa ndege wa Brussels - waliwafanyia upasuaji wagonjwa 15 katika kipindi cha masaa mawili baada ya milipuko hiyo.

Wafanyakazi wa afya waliona "mambo ya kutisha" ambayo walikuwa hawajawahi kuyaona hapo kabla, kwa mujibu wa Paul De Leyn, anayeongoza kitengo cha upasuaji wa koo na upasuaji jumla, na mwenzake Stefaan Nijs, anayesimamia upasuaji kiwewe.

Belgien Brüssel Paul De Leyn mit Kollege
Madaktari Nijs na De Leyn wana fahari ya ushirikiano kati ya wafanyakazi katika hospitali yao baada ya mashambuliziPicha: DW/K. Schuster

Misumari na vyuma kutoka kwa mabomu viliwadunga waathirika wengi. Wengi wao walichomeka sana na kuumia macho kutokana na mabomu hayo. "Ni wazi aliyefanya shambulizi hilo alinuia kusababisha uchungu mkubwa kadri alivyoweza kwa binadamu," Nijs alisema.

Hakuna kati ya madaktari hao aliyeweza kutoa kauli kuhusu mchakato wa kuwatambua wahanga, lakini walisema hospitali iliwasiliana na jamaa wa wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji kufikia saa sita usiku siku ya Jumanne.

Kuishi katika wakati

Mjini Brussels, mirundo ya mauwa, barua, maelezo na mishumaa imeongezeka nje ya malango ya kituo cha Maelbeek tangu siku ya shambulizi. Kufikia Ijumaa mvua ilikuwa imeufuta ujumbe upendo ana amani uliochorwa kwa chaki za rangi mbalimbali. "Kama watu wataniambia katika saa chache zijazo kwamba amekufa, nitalazimika kuishi na ukweli huo," alisema Duhaut.

Kwa Duhaut hisia ya huzuni inaibua kitendawili: amepokea ujumbe wa salamu nyingi za rambirambi, lakini bado anatumai rafiki yake atarejea. "Nina kumbukumbu nyingi sana nzuri na tumepitia mambo mengi pamoja. Hakuna anayeweza kuchukua hayo kutoka kwangu," alisema. "Ni muhimu kuishi katika wakati.""

Lisa Louis alichangia kuripoti kutoka Brussels

Mwandishi:Kathleen Schuster

Tafrisi:Josephat Charo

Mhariri:Isaac Gamba