1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na uanachama wa Uturuki

12 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCk3

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kupunguza mwendo wa majadiliano yanayohusika na bidii ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa sababu ya mgogoro wa Cyprus.Majadiliano pamoja na Uturuki juu ya mada 8 kutoka jumla ya 35,yatasitishwa kwa muda,hasa katika sekta za usafirishaji na biashara.Finland iliyoshika wadhifa wa urais wa Umoja wa Ulaya imesema,majadiliano hayatovunjwa lakini maendeleo yanayofanywa na Uturuki kutekeleza masharti yaliyotolewa,yatachunguzwa hadi mwaka 2009. Uturuki inashinikizwa kufungua bandari zake na viwanja vyake vya ndege kwa Cyprus,iliyojiunga na Umoja wa Ulaya mwaka 2004.Uturuki haiitambui serikali ya Cyprus ya Kigiriki.Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umesema huenda ukasita kuitenga kiuchumi Cyprus ya Kituruki iliyo kaskazini mwa kisiwa cha Cyprus.Kwa upande mwingine waziri wa nje wa Uturuki Abdullah Gul amesema,hatua ya kutaka kuchelewesha majadiliano ni ishara mbaya. Uamuzi wa mwisho unatarajiwa kupitishwa siku ya Alkhamisi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.