1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Tonny Blair katika harakati za kusaka amani mashariki ya kati

17 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBhg

Mjumbe mpya wa amani katika Mashariki ya Kati, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tonny Blair hii leo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na maafisa wa Umoja wa Ulaya, katika juhudi za jumuiya ya kimataifa kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Mkuu wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana ameondoka kwenda Mashariki ya Kati mara baada ya mazungumzo yake na Blair leo mchana.

Hapo jana Rais Georg Bush wa Marekani alitoa wito wa kufanyika kwa mkutano mkubwa wa kimataifa utakaoshirikisha Israel, Palestina na nchi za kiarabua kujaribu kufufua mazungumzo ya amani kati pande hizo mbili

Mjini Amman Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan aliupongeza wito huo wa Rais Bush, na kusema kuwa utafungua njia kuelekea kwenye mafanikio halisi ya amani kwenye eneo hilo.

Pia alisema kuwa hatua ya Rais Bush kutoa msaada wa dola millioni 190 kwa Palestina ni hatua madhubuti katika kuwasaidia wapalestina kujikwamua na dhiki za kimaisha zinazosababishwa na uchumi mbovu.

Wakati huo Ujerumani nayo imeupongeza wito huo wa Rais Bush wa kutaka kufanyika kwa mkutano wa amani ya mashariki ya kati.

Msemaji wa Serikali ya Ujerumani, Ulrich Wilhelm akizungumza mjini Berlin amesema kuwa Ujerumani inaunga mkono malengo hayo.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel hii leo alitarajiwa kuzungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu mpya wa serikali ya Palestina ya chama cha Fatah Salam Fayyad kumuhakikishia uungaji mkono wa Ujerumani kwa serikali hiyo.