1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Ulaya yasheherekea mkataba mpya

24 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBon

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano juu ya mfumo wa mkataba mpya wa mageuzi wa umoja huo.

Baada ya mazungumzo ya usiku kucha mjini Brussels Ubelgiji Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kwamba umoja huo umefikia muafaka mzuri juu ya mfumo wa upigaji kura ndani ya umoja huo ambao utaendelea kutumika hadi mwaka 2017.Poland ilitishia kuzuwiya kufikiwa kwa makubaliano hayo.

Nchi wanachama 27 wa umoja huo zimekubaliana kuujadili mkataba huo wa mageuzi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu na baadae kuuridhia ifikapo kati kati ya mwaka 2009.

Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye nchi yake iliikataa rasimu ya mkataba uliopita ameufurahia mkataba huo.

Amesema kitu muhimu kabisa ni kwamba mkataba wa katiba umewekwa kando na kuurudia mkataba wa kawaida ambapo mambo manne muhimu ambayo Uingereza ilikuwa ikiyataka ili kulinda msimamo wao yote yamekubalika.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso ameliambia gazeti la Jumapili la Ujerumani la Bild kwamba mkataba huo unaondowa mashaka juu ya uwezo wa Umoja wa Ulaya kuchukuwa hatua.