1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Umoja wa Ulaya washutumu kunyongwa kwa washirika wa marehemu Saddam

15 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCaJ

Umoja wa Ulaya umeshutumu kunyongwa kwa washirika wa marehemu Saddam Hussein kulikofanywa leo alfajiri. Serikali ya Irak imeonyesha ukanda wa video unaonyesha kunyongwa kwa Barzan al Tikriti, ndugu wa mama mmoja, wa marehemu Saddam Hussen, aliyekuwa kiongozi wa ujasusi wakati wa utawala wa Saddam, na Awadh Hamed al Bandar, aliyekuwa jaji mkuu.

Walihukumiwa kunyongwa pamoja na Saddam Hussein na mahakama ya mjini Baghdad mwezi uliopita kwa mauaji ya Washia 148 katika kijiji cha Dujail mnamo mwaka wa 1982.

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso amelaani vikali kunyongwa kwa watu hao akipinga hukumu ya kifo.

Msemaji wa serikali ya Irak, Ali al Daggagh ameutetea uamuzi wa kuwanyonga washirika hao wa Saddam Hussein.

´Watu hao walihusika pia na mauaji ya halaiki ya Wairaki mjini Anfal na Halabja na ukandamizaji wa uasi mnamo mwaka wa 1991. Mbali na hayo waliwatesa raia na kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu ndani ya Irak.´

Maofisa wa Irak wamesema sheria zote za kuwanyonga wafungwa zilifutwa kikamilifu safari hii lakini Barzan al Tikriti alikatwa kichwa wakati wa kutiwa kitanzi. Maiti za watu hao zimesafirishwa hadi mjini Tikrit leo alasiri kutumia helikopta ya jeshi la Marekani.